Guterres atishia kuipeleka Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141174-guterres_atishia_kuipeleka_israel_katika_mahakama_ya_kimataifa_ya_haki
Gazeti la Kizayuni limeripoti kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametishia kuupeleka utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague nchini Uholanzi.
(last modified 2026-09-03T09:08:50+00:00 )
Sep 03, 2026 09:04 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Gazeti la Kizayuni limeripoti kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametishia kuupeleka utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague nchini Uholanzi.

Gazeti la Kizayuni la " Israel Hayom" limeandika kwamba Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika barua yake kwa Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu, ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu shambulio la jeshi la Israel kwenye kituo cha mafunzo cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi na Ajira kwa Wapalestina (UNRWA) huko Qalandia kaskazini mwa Quds inayokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kwamba kituo hicho kina kinga ya Umoja wa Mataifa.

Askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel hivi majuzi walivamia jengo la UNRWA huko Qalandiya na kulikalia kwa siku nne, na kisha walivamia jengo hilo tena Jumapili iliyopita. Uvamizi huo ulifanyika ili kutekeleza sheria za Israel dhidi ya UNRWA na shughuli zake katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, ametangaza kwamba Umoja wa Ulaya hauwezi kukubali bidhaa zinazozalishwa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel na haupaswi kuunga mkono shughuli hizo kupitia biashara.

"Mlipuko wa vitendo vya kikatili ulioanzishwa na walowezi wenye msimamo mkali katika Ukingo wa Magharibi ni shambulio lisilokubalika dhidi ya utu wa watu wa Palestina," aliandika Jean-Noël Barrot katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, jana Jumatano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alisisitiza kuwa: "Umoja wa Ulaya hauwezi kuunga mkono shughuli hizo kupitia miamala ya kibiashara."