China na Iran zaahidi kupanua ushirikiano wa kimkakati katika nyanja zote
-
China na Iran zaahidi kupanua ushirikiano wa kimkakati katika nyanja zote
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholam-Hossein Mohseni Ejei, amesisitiza tena “azma” ya Iran ya kupanua uhusiano na China, akisisitiza kuwa ushirikiano imara wa kisheria na kimahakama unaweza kuwa nguzo ya mahusiano mapana ya kimkakati kati ya nchi hizo mbili.
Ejei alitoa kauli hizo siku ya Ijumaa wakati wa mkutano na Zhang Jun, Rais wa Mahakama ya Juu ya Watu wa China na afisa mkuu wa mahakama nchini humo, pembezoni mwa mkutano wa viongozi wa mahakama wa nchi za BRICS jijini New Delhi, India.
Pia amesisitiza ushirikiano wa kiteknolojia, hususan matumizi ya akili mnemba (AI) na teknolojia za kidijitali katika masuala ya kimahakama, akisema uwezo wa kisayansi na kiteknolojia wa China, ukiunganishwa na uwezo wa ndani wa Iran, unaweza kufungua njia mpya za ushirikiano wa nchi mbili.
Kwa upande wake, Zhang Jun amesema mahakama ya China ina nia ya kuimarisha ushirikiano na mwenzake wa Iran, hasa katika utawala wa kimahakama, akili mnemba na teknolojia za kidijitali. Pia aliusifu ustahimilivu wa wananchi wa Iran wakati wa vita vya hivi karibuni na kueleza matumaini kwamba mahusiano kati ya China na Iran yatapanuka katika nyanja zote.
Kauli za Ejei zilikuja wakati wa ziara yake nchini India kwa ajili ya mikutano ya viongozi wa mahakama wa BRICS. Iran ilijiunga na BRICS katika miaka ya hivi karibuni pamoja na wanachama wengine wapya, wakiwemo Misri, Ethiopia, Indonesia na Umoja wa Falme za Kiarabu. Wanachama wengine wa BRICS ni Brazil, Russa, India, China na Afrika Kusini.
Katika mkutano mwingine tofauti jijini New Delhi na wasomi wa Kiislamu na viongozi wa jumuiya mbalimbali za kidini, Ejei amewataka viongozi wa kidini na watu mashuhuri duniani kote kushirikiana ili kukuza amani ya kimataifa, haki na ustawi. Akiashiria mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, Ejei ametolea mfano shambulio la Februari 28 dhidi ya shule ya msingi ya Shajareh Tayyebeh huko Minab, katika Mkoa wa kusini wa Hormozgan, akisema shambulio hilo liliua makumi ya watoto, walimu na raia wengine.
Amelielezea tukio hilo kama mfano mmoja wa yale aliyoyaita jinai zilizoenea wakati wa uchokozi wa siku 40 wa Marekani na Israel, akisema kuwa makumi ya shule, hospitali, vituo vya utamaduni na miundombinu ya kitaifa na kidini pia vililengwa.
Ejei pia amekosoa kimya cha jumuiya ya kimataifa kuhusu vita vya Gaza, akisema wanawake na watoto wameuawa na idadi kubwa ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao. Mkuu huyo wa mahakama ya Iran ametoa wito wa juhudi za pamoja za kuleta amani na kuboresha hali ya maisha duniani kote, akisema Iran inataka “amani na ustawi kwa wanadamu wote” katika ulimwengu usio na ubaguzi, unyonyaji na ukoloni.