Sep 04, 2026 06:01 UTC
  • Ijumaa, 4 Septemba, 2026

Leo ni Ijumaa tarehe 22 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1448 Hijria, sawa na tarehe 4 Septemba 2026.

Siku kama ya leo miaka 1444 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (saw).

Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakutakiwa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla.

Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao.   ****

Siku hii ya leo tarehe 13 Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi Abu Raihan Muhammad bin Ahmad Kharazmi Biruni msoni mtajika wa Iran na Ulimwengu wa Kiislamu.

Abu Raihan Biruni alizaliwa katika mji wa Birun karibu na Kharazm, moja kati ya miji ya zamani ya Iran.  Abu Raihan Biruni alikuwa mtaalamu katika elimu za historia, jiografia unajimu na hisabati. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mazungumzo na maulama na watawala wa zama hizo na baada ya kujifunza lugha ya Sanskrit ambayo ni lugha ya kale ya Kihindi. Alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind'.

Mbali na kitabu hicho msomi huyo ameandika vitabu vingi katika nyanja tofauti zikiwemo za unajimu na mantiki.   ****

Siku kama ya leo miaka 144 iliyopita, mota ya kwanza ya umeme ilitengenezwa.

Mvumbuzi na mtengenezaji wa mota hiyo alikuwa Thomas Edison mtaalamu na mtafiti wa Kimarekani. Kwa kutumia mota hiyo ya umeme, Edison alianzisha kiwanda cha umeme katika mji wa New York na wakati huo huo akawa amefanikiwa kudhamini sehemu ya mahitaji ya mwanga katika mji huo. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwamba, mwaka 1879, Edison alifanikiwa kuvumbua balbu.     ***

Tarehe 4 Septemba miaka 118 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Marekani mwenye asili ya Afrika, Richard Wright.

Baada ya mashaka makubwa maishani, Richard Nathaniel Wright alianza kazi ya uandishi akiwa na umri wa miaka 30. Baadhi ya vitabu vyake vinaakisi sehemu ya maisha ya kifukara na ya kuchosha ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Ameandika vitabu vingi kama Black Boy, Native Son, Uncle Tom's Children na The Outsider.   ***

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin.

Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu wa nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 Miladia katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland.

Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasiwasi mkubwa.     ***

Na tarehe 13 Shahrivar miaka 48 iliyopita kulifanyika maandamano ya kwanza ya mamilioni ya Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.

Maandamano hayo yalianza baada ya Swala ya Eid-ul-Fitr kutoka sehemu nne za Tehran. Waandamanaji waliokuwa wamebeba picha kubwa ya Imam Ruhullah Khomeini (RA), kiongozi wa hayati wa Mapinduzi ya Kiislamu, walipaza sauti na nara za kudai uhuru, kujitawala na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran.

Maandamano hayo makubwa ya mamilioni, ambayo yalikuwa msingi wa maandamano ya kihistoria ya tarehe 17 Shahrivar ya mwaka huo huo, yalimalizika baada ya Sala ya jamaa ya adhuhuri.