Umoja wa Mataifa waonya ‘El Nino kubwa’ inayoweza kuvunja rekodi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141212-umoja_wa_mataifa_waonya_el_nino_kubwa’_inayoweza_kuvunja_rekodi
Shirika la Hali ya Hewa Duniani limetangaza kuwa, El Niño inayoendelea kuimarika inaweza kuwa kali zaidi kuwahi kurekodiwa, ikiongeza hatari ya mafuriko, ukame, joto kali na upungufu mkubwa wa chakula.
(last modified 2026-09-05T03:16:07+00:00 )
Sep 05, 2026 03:15 UTC
  • Umoja wa Mataifa waonya ‘El Nino kubwa’ inayoweza kuvunja rekodi
    Umoja wa Mataifa waonya ‘El Nino kubwa’ inayoweza kuvunja rekodi

Shirika la Hali ya Hewa Duniani limetangaza kuwa, El Niño inayoendelea kuimarika inaweza kuwa kali zaidi kuwahi kurekodiwa, ikiongeza hatari ya mafuriko, ukame, joto kali na upungufu mkubwa wa chakula.

Kwa mujibu wa shirika hilo, kuna uwezekano wa karibu asilimia 100 kwamba El Niño hiyo itaendelea hadi Februari 2027. Inatarajiwa kufikia kilele chake mwishoni mwa mwaka huu, ingawa athari zake kwa hali ya hewa zinaweza kuendelea kuonekana katika sehemu mbalimbali za dunia hadi katika mwaka ujao 2027.

Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Celeste Saulo amesema mjini Geneva Uswisi kwamba,"Endapo mwenendo huu utaendelea, inaweza kuwa kali kuliko tukio lolote tangu tulipoanza ufuatiliaji,”. Aidha amesema shirika hilo tayari limeiweka katika kiwango cha "kali sana”, ambacho ndicho cha juu zaidi katika vipimo vyake vinne.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema El Niño hiyo inakuwa kubwa zaidi mbele ya macho ya dunia. Ameonya kuwa sayari imeingia katika eneo lisilofahamika vizuri, huku joto la bahari na la anga likiendelea kupanda.

Guterres amesema, El Niño inaongezwa ukubwa mbele ya macho yetu. "Sayansi haiachi nafasi ya shaka: Sayari iko katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, maji yanaendelea kupata joto na dunia imeingia katika eneo la hatari la hali mbaya ya hewa.”

Kwa kawaida, El Niño hutokea baada ya kipindi cha miaka miwili hadi saba na hudumu kwa takriban miezi tisa hadi 12. Hupishana na La Niña, hali ambayo maji katika eneo hilo la Pasifiki huwa baridi kuliko kawaida. Kati ya vipindi hivyo viwili hujitokeza hali inayotajwa kuwa ya kawaida au isiyoegemea upande wowote.