Sep 05, 2026 02:52 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumamosi 23 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1448 Hijria mwafaka na 5 Septemba 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1247 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatima Maasuma, dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as), aliwasili katika mji wa Qum, Iran. Mwaka mmoja baada ya safari ya kubaidishiwa kaka yake huko katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kutoka Madina kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka na Imam wake huko Khorasani. Baada ya kuwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (saw). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake, Imam Ridha (as), Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Hii leo Haram ya mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw), Bibi Fatma Maasuma (as), katika mji wa Qum ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya dunia huenda kufanya ziara katika eneo hilo.

***

Siku kama hii ya leo miaka 169 iliyopita alifariki dunia Auguste Comte mwanafalsafa na mwanahisabati wa Kifaransa. Comte alizaliwa mwaka 1798. Alishirikiana kwa muda fulani huko Paris na Henri de Saint Simon, mwanafalsafa mashuhuri wa zama hizo na baadaye Comte alianza kufundisha. Auguste Comte alikuwa mwasisi wa mfumo wa elimu jamii. Comte ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha The Positive Philosophy of Auguste Comte.

***

 Miaka 139 iliyopita mwafaka na tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1887, mto mkubwa wa Huang He huko China ulianza kufurika maji. Mafuriko hayo makubwa yalisababishwa na kujaa maji katika mto huo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Zaidi ya watu laki tisa walipoteza maisha katika mafuriko hayo na taathira zake mbaya. Aidha miji kadhaa, mamia ya vijiji na mashamba mengi yaliharibiwa baada ya kukumbwa na mafuriko ya mto Huang He huko China. 

***

Miaka 121 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 5 Septemba mwaka 1905, Mkataba wa Portsmouth ulitiwa saini na hivyo kuhitimisha vita kati ya Russia na Japan. Februari 8 mwaka 1904, vikosi vya majeshi ya Japan vilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya meli za kivita za Russia na kuyadhibiti maeneo ya Manchuria ambayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Russia. Russia ilipata vipigo mfululizo katika vita hivyo. Hatimaye kwa upatanishi wa Marekani, katika siku kama ya leo pande mbili zilitia saini mkataba wa Portsmouth na huo ukawa mwisho wa vita kati ya Japan na Russia. 

***

 Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita sawa na 14 Shahrivar 1360 Hijria Shamsia, Ayatullah Ali Quddusi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mapinduzi ya Kislamu nchini Iran aliuawa shahidi katika mlipuko wa bomu lililotegwa na kundi la kigaidi la MKO. Shahidi Quddusi alipata elimu yake kutoka kwa wasomi na wanavyuoni kama Ayatullah Burujerdi, Allama Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA na kufikia daraja ya Ijtihad. Shahidi Quddusi alishiriki vilivyo katika masuala ya kidini na mfano wa wazi wa mchango wake ni kuasisi skuli ya mafunzo ya kidini ya Haqqani. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alisimama kupambana na utawala dhalimu wa Shah na akatiwa jela kwa kipindi fulani. Ayatullah Quddusi alisabilia miaka ya mwishoni mwa umri wake katika juhudi za kuimarisha mfumo mchanga wakati huo wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye aliuawa shahidi na magaidi wa kundi la MKO katika siku kama hii ya leo.

***

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Septemba 1993, moja ya misikiti ya kustaajabisha na ya kuvutia katika Ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco. Msikiti huo umejengwa kwa mtindo wa kisasa na una minara inayoakisi usanifu majengo wa hali ya juu wa Kiislamu. Eneo la uwanja wa msikiti huo lina uwezo wa kuchukua waumini 75,000. Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba kubwa na Chuo Kikuu cha Kidini. Msikiti huo unahesabiwa kuwa moja ya misikiti mikubwa na maridadi sana katika Ulimwengu wa Kiislamu.

***