Qalibaf: Marekani inapaswa kujua kwamba enzi ya "majibu sawia" imekwisha
-
Mohammad Baqir Qalibaf
Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa kabla ya kuchelewa, Wamarekani wanapasa kujua kwamba kanuni za mchezo zimebadilika na kuanzia sasa, uchokozi wowote dhidi ya maslahi na usalama wa Iran utajibiwa kwa hatua itakayokuwa "ya haraka zaidi, nzito zaidi na yenye kuumiza zaidi."
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Mohammad Baqir Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema katika hotuba yake kabla ya kuanza kikao cha wazi cha Buge leo Jumapili kwamba siku hizi zinakumbusha hamasa ya kihistoria ya wananchi wa Tehran ya tarehe 17 mwezi Shahrivar na "Ijumaa Nyeusi" hapo mwaka 1978.
Siku hiyo damu safi ya wananchi ilimwagwa ardhini katika uwanja wa Shohada jijini Tehran na utawala wa kibaraka wa Pahlavi ikimwagilia mche wa Mapinduzi ya Kiislamu na kudhihirisha kuwa taifa hili halitasita kusabilia maisha katika njia ya kweli na katika kusimama imara dhidi ya uistikbari na madola ya kibeberu.
Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa: Uwanja wa mapambano leo hii umesalia uleule, na tuko kwenye njia ya 'Jihad' na mapambano ya kusimama kidete; na katika hali ambayo adui ametumia nguvu zake zote kulishinikiza taifa la Iran tutamfedhehesha na kumshinda vibaya katika vita vya kiuchumi kama tulivyofanya katika nyanja za mapambano ya kijeshi na kidiplomasia kupitia juhudi za kina za nguzo za taifa na istiqama isiyo na kifani ya wananchi na kwa neema ya Mwenyezi Mungu.
Spika wa Bunge la Iram amesema: Msimamo huu thabiti na kudumisha uwezo wa makabiliano unashuhudiwa katikati ya vita kamili dhidi ya kambi nzima ya ukafiri kufuatia vipigo vikali vilivyotolewa na vikosi vya ulinzi dhidi ya kambi za Marekani ambapo viongozi wa nchi hiyo wamefikia hali ya kukata tamaa na kuamua kutumia maneno chapwa na kaulimbiu tupu, huku wakitumia akili bandia kutengeneza picha na video kutoka uwanja wa vita.