Jimbo la Plateau nchini Nigeria lafunga shule kutokana na mlipuko wa Diphtheria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141244-jimbo_la_plateau_nchini_nigeria_lafunga_shule_kutokana_na_mlipuko_wa_diphtheria
Serikali ya Jimbo la Plateau linalopatikana kaskazini-kati mwa nchi ya Nigeria imeamuru kufungwa kwa muda usiojulikana shule za serikali na za watu binafsi za msingi na sekondari kuanzia tarehe 7 mwezi huu wa Septemba kutokana na kuenea ugonjwa wa diphtheria katika maeneo manne ya serikali za mitaa katika jimbo hilo.
(last modified 2026-09-06T11:29:28+00:00 )
Sep 06, 2026 11:26 UTC
  • Jimbo la Plateau nchini Nigeria lakumbwa na Diphtheria
    Jimbo la Plateau nchini Nigeria lakumbwa na Diphtheria

Serikali ya Jimbo la Plateau linalopatikana kaskazini-kati mwa nchi ya Nigeria imeamuru kufungwa kwa muda usiojulikana shule za serikali na za watu binafsi za msingi na sekondari kuanzia tarehe 7 mwezi huu wa Septemba kutokana na kuenea ugonjwa wa diphtheria katika maeneo manne ya serikali za mitaa katika jimbo hilo.

Diphtheria ni ugonjwa mbaya unaosababishwa na bakteria ambao huathiri utando wa pua na koo.

Joyce Ramnap, Kamishna wa Jimbo la Plateau anayeshughulikia masuala ya habari na mawasiliano amesema kuwa agizo hili linahusu shule ambazo tayari zimeanza tena shughuli za masomo na kwamba hatua hiyo itaendelea kutekelezwa hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine.

Serikali imesema kuwa wagonjwa kadhaa wameripotiwa katika maeneo ya serikali za mitaa ya Jos North, Jos South, Bassa na Wase, jambo lililopelekea kufungwa kwa maeneo hayo kama hatua ya tahadhari ya kuzuia kuenea ugonjwa huo.

Wamiliki wa shule, wasimamizi na walimu wameelekezwa kutii agizo hilo. Wazazi na walezi pia wamehimizwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanabaki nyumbani wakati huu ambapo shule zimefungwa.  

Haya yanajiri huku hali ya ugonjwa wa Diphtheria ikizidi kuwa mbaya katika jimbo la Plateau. Kamishna wa Afya wa jimbo hilo, Nicholas Baamlong alisema mapema wiki hii kuwa watu 23 wamefariki dunia na visa 143 vinavyoshukiwa kuwa vya ugonjwa huo vikiripotiwa, huku wagonjwa tisa wakipata matibabu katika Hospitali ya Mafunzo ya Chuo Kikuu cha Jos na Hospitali Maalumu ya Plateau.

Baamlong ametaja uhaba wa dawa ya kukabiliana na sumu ya ugonjwa wa diphtheria yaani (diphtheria antitoxin) na wagonjwa kuchelewa kufika katika vituo vya afya kuwa changamoto kuu katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo.

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Nigeria (NCDC) kimearifiwa kuhusu mlipuko huo huku serikali ya jimbo la Plateau ikitarajia msaada kutoka serikali kuu. Misaada inayohitajika sasa ni pamoja na shehena ya dawa ya kukabiliana na sumu (antitoxin) na vifaa maalumu vya kukusanyia sampuli.