Nigeria yaagiza kufanyika msako baada ya kutekwa nyara watu wengi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140988-nigeria_yaagiza_kufanyika_msako_baada_ya_kutekwa_nyara_watu_wengi
Rais Bola Tinubu wa Nigeria ameviagiza vyombo vya usalama kuwasaka watu wenye silaha wanaotuhumiwa kuua makumi ya watu na kuwateka nyara wakazi wa vijiji vinne katika jimbo la Niger linalopatikana kaskazini- kati nchini humo.
(last modified 2026-08-27T04:24:08+00:00 )
Aug 27, 2026 04:22 UTC
  • Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria
    Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria

Rais Bola Tinubu wa Nigeria ameviagiza vyombo vya usalama kuwasaka watu wenye silaha wanaotuhumiwa kuua makumi ya watu na kuwateka nyara wakazi wa vijiji vinne katika jimbo la Niger linalopatikana kaskazini- kati nchini humo.

Mashambulizi hayo yalijiri Ijumaa iliyopita katika eneo la mbali la Borgu, karibu na mipaka ya Nigeria na Benin na majimbo ya Kebbi na Kwara.

Wakazi wa vijiji hivyo katika jimbo la Niger wameeleza kuwa misikiti kadhaa ilishambuliwa kwa wakati mmoja huku watu wakiwa katika ibada. Kiongozi mmoja wa vijana wa eneo hilo ameeleza kuwa kuna uwezekano watu wasiopungua 500 wametekwa nyara na washambuliaji ingawa idadi hiyo haijathibitishwa na vyanzo huru vya habari.

Ukubwa wa matukio ya utekaji nyara umedhihirika zaidi baada ya washambuliaji kusambaza video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha kundi la watu walioketi msituni.

Watekaji nyara hao wamedai kuwa watu walioonekana kwenye video hiyo ni miongoni mwa wale waliotekwa wakati wa mashambulizi ya Ijumaa iliyopita dhidi ya vijiji vine katika jimbo la Niger.

Kwa baadhi ya familia, picha hizo zimetoa ishara ya kwanza kwamba ndugu zao waliotekwa nyara bado wangali hai hata hivyo familia nyingine hadi sasa hazina taarifa zozote kuhusu ndugu zao waliopotea.

Msemaji wa polisi Wasiu Abiodun, ameviambia vyombo vya habari kuwa kuwa zaidi ya watu 40 wameuawa, ingawa mamlaka husika katika jimbo la Niger bado hazijabaini idadi kamili ya waliouawa katika hujuma ya watu wenye silaha.

Imeelezwa kuwa washambuliaji walikuwa wamevaa mavazi ya kijeshi na kuvamia vijiji vya Dekara, Gidan Zana, Sabon Gida na Masaka.