Iran yaiambia Jordan: Mnataraji tusubiri hadi lini kutomjibu mchokozi?!
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu matamshi ya hivi karibuni ya waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Jorda kwa kumuuliza: Mnataraji Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isubiri hadi lini kutomjibu mchokozi ambaye haheshimu haki ya kujitawala nchi za Kiarabu wala haki za Iran?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman al-Safadi amelalamikia majibu yanayotolewa na Iran kwa mashambulizi yanayofanywa na Marekani dhidi ya ardhi ya Iran kutokea katika ardhi ya Jordan. Malalamiko hayo yamepata majibu ya haraka ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araqchi.
Araqchi amesema leo Ijumaa kwamba: Sijui kwa mtazamo wa wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kusubiri kwa muda gani kumjibu mchokozi ambaye haheshimu uhuru wa nchi za Kiarabu wala haki ya kujitawala Iran?
Aidha amehoji kwa kusema: Je, (Waziri wa Mambo ya Nje wa Jorda) kweli hajui kwamba mashambulizi ya kwanza ya Marekani, yaliyotumia anga, ardhi na maji ya nchi za Kiarabu, yalisababisha mauaji ya Wairani wasio na hatia?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman Safadi amedai katika taarifa kwamba Iran ilishambulia Jordan na nchi nyingine katika eneo hili saa mbili baada ya vita kuanza, na kwamba shambulio hilo halikuwa jibu la jinai za Marekani. Pia amedai kwamba Jordan itafanya kila iwezalo kulinda usalama wake, raia na uhuru wake.
Baada ya jeshi la Marekani kushambulia sehemu fulani za Kisiwa cha Lark jioni ya Jumapili, Agosti 30, 2026 na kuua shahidi na kujeruhi raia kadhaa wa Iran, vikosi vya ulinzi vya Iran vilijibu jinai hiyo kwa kupiga kambi za kijeshi za Marekani huko Jordan.
Lakini viongozi wa Jordan badala ya kuilaumu Marekani na kuizuia isitumie ardhi yake kushambulia nchi nyingine, ndio kwanza wanalalamikia majibu yanayotolewa na Iran ya jinai inazofanyiwa kupitia anga, ardhi na maji ya nchi za Kiarabu.