Sayyid Khatami: Vita vya leo dhidi ya Iran ni vita mseto
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, hivi sasa Iran inakabiliwa na vita mseto kutoka kwa adui na kwamba hata vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Waislamu vilianza tangu enzi za Mtume Muhammad SAW mwanzoni mwa Uislamu.
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ametoa ushahidi wa Qur'ani Tukufu kuthibitisha kwamba mashinikizo ya kiuchumi na kuzingirwa si suala jipya na wala Trump si wa kwanza kulileta kwani mashinikizo kama hayo yamekuwepo tangu mwanzoni mwa Uislamu.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami vilevile amesema kuwa, vita vya leo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni "vita mseto vyenyewe hasa" na kuongeza kuwa, sehemu yake moja ni vita vya kijeshi ambavyo bado vinaendelea na vinaendeshwa na mtu katili na mwoga ambaye haheshimu kabisa sheria.
Amesema: "Watoto 168 wa shule ya msingi wana makosa gani? Wanalindwa na sheria zote za dunia. Wanamichezo wana madhambi gani?" Unageuza harusi za watu kuwa maombolezo. Vita hivi ni vita vya mtu mwoga."
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran pia amesisitiza kwa akusema: Tab'an vikosi vya ulinzi vya Iran vitaendelea kutoa majibu kwa njia bora, kwa ushujaa na bila ya woga.
Akigusia jinsi makamanda na wafanyakazi wa Jeshi la Ulinzi wa Anga la Iran walivyokuwepo kwenye ibada hiyo ya Sala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran, Sayyid Khatami amesema: Leo pia, maafisa wapendwa wa Jeshi la Ulinzi wa Anga la Jamhuri ya Kiislamu na kamanda wao anayeheshimika wameshiriki katika ibada hii ya Sala ya Ijumaa. Hawa ni mikono yenye nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aidha amesema: Mbali na vita vya kijeshi, kuna pia vita vya kiuchumi. Tab'ani adui amekuwa akipigana vita vya kiuchumi dhidi yetu tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Sambamba na hayo, kuna vita vya vyombo vya habari na kueneza uongo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu pamoja na vita vya kiutamaduni dhidi ya taifa la Iran.