Sep 27, 2026 14:06 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili 15 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria mwafaka na 27 Septemba 2026 Miladia.

Miaka miwili iliyopita, katika siku kama ya leo, tarehe 27 Septemba 2024 Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, aliuawa shahidi.

Sayyid Hassan Nasrallah alizaliwa tarehe 8 Shahrivar 1339 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 31 Agosti 1960, katika moja ya maeneo ya mashariki mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Baba yake aliitwa Sayyid Abdulkarim, na mama yake alikuwa Nahdiya Safiuddin, ambao walitokea katika kijiji cha Al-Bazouriya, kusini mwa Lebanon, kabla ya kuhamia Beirut. Nasrullah alikuwa mtoto wa kwanza katika familia yao, akiwa na kaka watatu na dada watano.

Baada ya kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon mwaka 1975, familia yake ilirejea katika kijiji cha Al-Bazouriya, ambako aliendelea na masomo yake ya sekondari katika mji wa Tiro.

Tangu akiwa kijana, Sayyid Hassan alivutiwa na masomo ya kidini katika hawza. Mwaka 1976 alikwenda Najaf, Iraq, ili kuendelea na masomo ya kidini. Alikuwa mwanafunzi wa Sayyid Abbas al-Musawi, na kwa kipindi fulani pia alihudhuria masomo ya Sayyid Mahmoud Hashemi, Sayyid Kazem Haeri na Muhammad Fazel Lankarani mjini Qom, Iran.

Kuanzia mwaka 1975 hadi 1982, alikuwa mwanachama wa Harakati ya Amal ya Lebanon. Hata hivyo, mwaka 1982 alijitenga na harakati hiyo pamoja na kundi la wanazuoni wapiganaji na kuanzisha Hizbullah ya Lebanon.

Baada ya kuuawa shahidi kwa Sayyid Abbas al-Musawi tarehe 16 Februari 1992, Nasrullah akiwa na umri wa miaka 32 alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa tatu wa Hizbullah, nafasi ambayo aliendelea kushikilia hadi mwisho wa maisha yake.

Katika kipindi cha uongozi wake, Hizbullah iligeuka kuwa nguvu muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati na kupata mafanikio kadhaa ya kihistoria. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuondolewa kwa vikosi vya Israel kutoka kusini mwa Lebanon mwaka 2000, kuachiliwa kwa wafungwa wa Lebanon na kurejeshwa kwa miili ya wapiganaji wa Muqawama mwaka 2004, pamoja na kile Hizbullah ilichokitaja kuwa ushindi katika vita vya siku 33 vya mwaka 2006.

Katika maisha yake ya kisiasa, Sayyid Hassan Nasrullah alikuwa na uhusiano wa karibu na kile kinachojulikana kama mhimili wa Muqawama pamoja na viongozi wa Iran. Alijulikana kama mshirika wa karibu wa Iran na mpinzani mkubwa wa Israel.

Nasrullah alilengwa mara kadhaa katika njama za kumuua zilizohusishwa na Israel, zikiwemo mwaka 2004, 2006 na 2011, lakini majaribio hayo hayakufanikiwa.

Hatimaye, tarehe 27 Septemba 2024, Sayyid Hassan Nasrullah aliuawa shahidi kufuatia mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa na Israel katika eneo la Dahieh, kusini mwa Beirut.

Tarehe 27 Septemba inasadifiana na Siku ya Kimataifa ya 'Utalii. Utalii ni moja ya sekta muhimu za mabadilishano ya kiutamaduni baina ya watu wa mataifa mbalimbali. Aidha utalii unaweza kutimia kupitia safari na utalii wa ndani na nje ya nchi kwa madhumuni tofauti. Licha ya kwamba utalii umekuwa na historia ya muda mrefu katika maisha ya mwanadamu, lakini utalii wa mfumo wa kisasa ulianza mwanzoni mwa karne ya 16, wakati yaliposhika kasi mapinduzi ya kiviwanda barani Ulaya na kuvumbuliwa aina mpya ya maisha barani humo.

***

Siku kama leo miaka 30 iliyopita, kundi la Taliban lilivamia na kutwaa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Kundi la Taleban liliasisiwa mnamo mwaka 1994 na likateka hatua kwa hatua maeneo ya kusini na magharibi mwa Afghanistan kwa himaya ya Marekani, misaada ya kisiasa na kijeshi ya Pakistan pamoja na misaada ya kifedha ya Saudi Arabia. Jeshi la serikali ya Afghanistan lililokuwa likiongozwa na Ahmad Shah Mas'ud liliondoka mjini Kabul siku moja kabla ya Taliban kuuteka mji huo. Baada ya kuingia Kabul, kundi la Taliban lilianza kutekeleza sheria kali na zinazoshabihiana na zile za karne za kati dhidi ya wananchi.

***

Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, mji wenye jamii kubwa ya watu wa Beijing ulichaguliwa rasmi kuwa mji mkuu wa China. Mji wa kihistoria wa Beijing unapatikana mashariki mwa nchi hiyo na unahesabiwa kuwa moja ya vituo vikubwa vya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni nchini China. Beijing ilichaguliwa kuwa mji mkuu wa China baada ya Mao Tse-tung kuchukua madaraka ya nchi na kiongozi wa wakati huo wa China Chiang Kai-shek kulazimika kukimbilia Taiwan.

***

Miaka 86 iliyopita, katika siku kama ya leo, tarehe 27 Septemba 1940: “Mkataba wa Chuma” ulisainiwa kati ya nchi waitifaki katika Vita vya Pili vya Dunia. Mkataba huo, uliounganisha miji mikuu mitatu ya Roma, Berlin na Tokyo katika mhimili mmoja, ulisainiwa kati ya Ujerumani ya Kinazi, Italia na utawala wa Japan. Kutokana na mkataba huo, nchi hizo tatu zilijulikana katika Vita vya Pili vya Dunia kama Nchi za Mhimili. Miongoni mwa matokeo yaliyohusishwa na mkataba huo ni shambulio la Japan dhidi ya Marekani na kuingia Marekani katika Vita vya Pili vya Dunia.

***

Miaka 155 iliyopita, katika siku kama ya leo, tarehe 27 Septemba 1871: Grazia Deledda, mwandishi mahiri wa hadithi kutoka Italia na mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi, alizaliwa. Hadithi zake, ambazo kwa kiasi fulani zinaweza kuchukuliwa kuwa wasifu wa kubuni, zinaakisi tofauti za tabia na haiba za wanadamu. Sambamba na kuandika riwaya ndefu, Deledda pia aliandika hadithi fupi kwa ajili ya magazeti na majarida. Miongoni mwa kazi zake maarufu ambazo zilitafsiriwa katika lugha mbalimbali za Ulaya ni “Upepo wa Chuki,” “Baada ya Talaka,” “Njiwa na Mwewe,” “Ngoma ya Mkufu,” “Kuelekea Kushoto,” “Majivu,” na nyinginezo. Grazia Deledda alikuwa mmoja wa waandishi mashuhuri wa fasihi ya Italia, na mwaka 1926 alitunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi.

***