Sep 23, 2026 03:49 UTC
  • Jumatano, Septemba 23, 2026

Leo ni Jumatano mwezi 11 Mfunguo Saba Rabiul Thani 1448 Hijria mwafaka na 23 Septemba 2026 Miladia.

Miaka 351 iliyopita katika siku kama ya leo, Valentin Conrart mwandishi na mwanafasihi wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 72.

Alizaliwa mwaka 1603 katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na fasihi ya lugha na kwa msingi huo ndio maana alipokuwa katika rika la ujana, Valentin Conrart akawa na mapenzi na taaluma ya fasihi ya lugha na taratibu akaanza kujihusisha na fani ya uandishi.

@@@

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita sawa na Septemba 23 mwaka 1932, Saudi Arabia iliasisiwa, na Abdulaziz bin Saud akawa mfalme wa nchi hiyo. Bara Arabu au Hijaz ni mahali alipotokea Mtume wa Uislamu Muhammad S.A.W. Saudi Arabia ilijitoa chini ya udhibiti wa utawala wa Abassiya mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria na hadi karne kadhaa badaye, nchi hiyo iliendelea kuwa na ukosefu wa amani.

Jitihada za al Saud za kutaka kuiongoza Saudia zilianza katikati mwa karne ya 18 na kushika kasi zaidi mwanzoni mwa karne ya 20.

@@@

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, aliaga dunia Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili raia wa Austria.

Sigmund alizaliwa mwaka 1856. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba binadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili.

Kwa sababu hiyo anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis.

@@@@

Katika siku kama ya leo miaka 124 iliyopita sawa na tarehe Mosi Mehr 1281 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu, aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake.

Baada ya kukamilisha masomo ya msingi, Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa ya kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na hatimaye Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Wakati wa uongozi wake wa miaka kumi, Imam Khomeini aliongoza Mapinduzi kupitia misukosuko mizito ya baada ya ushindi wa Mapinduzi na katika kipindi chote cha vita, huku akipaza sauti ya kudai haki na uadilifu mbele ya nguvu za Istikbari. Hatimaye, shujaa huyu wa Jihadi na kielelezo cha elimu na utendaji, tarehe 14 Khordad mwaka 1368 (sawa na Juni 3, 1989) akiwa na umri wa miaka 88, alirejea kwa Mola wake. Baada ya mazishi ya kipekee yasiyo na kifani duniani, alizikwa katika makaburi ya Behesht-e Zahra mjini Tehran.

@@@

Mosi ya Mehr kwa kalenda ya Hijria Shamsia nchinii Iran sawa na 23 Septemba mwaka huu ni Siku ya Kufunguliwa kwa Shule na Siku ya Kitaifa ya Bendera

Tarehe Mosi  Mehr nchini Iran, si mwisho tu wa likizo za miezi mitatu ya kiangazi na kuanza kwa muhula mpya wa masomo, bali ni siku yenye uzito wa pekee. Mwaka huu, mosi ya Mehr si mwanzo tu wa kurejea madarasani kwa wanafunzi; katika kalenda rasmi ya nchi, siku hii imetambuliwa kama “Siku ya Bendera”, ishara ambayo inapita rangi na picha zake, na kuwa kielelezo cha historia, ardhi, mamlaka, na utambulisho wa pamoja wa taifa.

Kwa mataifa mengi, bendera ni sehemu ambapo tofauti za kikabila, lugha, kidini, na kiutamaduni huwekwa pembeni ili kutoa nafasi kwa fikra moja kuu ya “Uzalendo.” Kuipa jina mosi ya Mehr kama “Siku ya Bendera” nchini Iran ni fursa kwa kizazi kipya kufahamu vyema ishara hii ya kitaifa na kuimarisha hisia ya utambulisho na mapenzi kwa ardhi yao. Kuambatana kwa tukio hili na kufunguliwa kwa shule kuna maana kubwa; wanafunzi wanapoingia shuleni katika siku hii, si tu wanaanza safari ya kutafuta elimu, bali pia wanapata fursa ya kuzama zaidi katika historia, utamaduni, na alama za utambulisho wao wa kitaifa, wakijenga uhusiano wa kina na nchi yao.

Katika mwaka huu wa 1405 Hijria Shamsia, tukio hili limepata maana tofauti zaidi. Katika miezi iliyofuata baada ya vita na mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, bendera ya Iran imekuwa na uwepo mkubwa katika mikusanyiko mingi na programu za kijamii, huku kupeperushwa kwa bendera kugeuka kuwa moja ya dhihirisho kuu la umma katika mikusanyiko hiyo.

Kwa mtazamo huu, bendera si alama rasmi inayopepea juu ya majengo ya serikali pekee; bali ni lugha ya taswira ya utambulisho kwa nchi na kumbukumbu ya pamoja ya kihistoria. Pale watu wanaposhikilia bendera hiyo katika siku za majaribu na misukosuko, ishara hii inakuwa ni sauti ya mshikamano, utambulisho wa kitaifa, na msisitizo thabiti wa kulinda ardhi na uhuru wa nchi.