Jumanne 22 Septemba 2026
Leo ni Jumanne, 10 Rabiul Thani 1448 Hijria mwafaka na 22 Septemba 2026 Miladia.
Miaka 1247 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Jaafar al-Kadhim (as), ambaye ni miongoni mwa Ahul Bayt wa Mtume Muhammad (SAW).
Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu.
Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) kuwasili Khurasan nchini Iran, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake, lakini akiwa njiani alisimama katika mji wa Qum na kufariki dunia mjini humo kutokana na maradhi au kwa mujibu wa kauli nyingine, kutokana na sumu aliyeopewa.
Kaburi au Haramu tukufu ya binti wa Imam Musa al-Kadhim (a.s) jijini Qom ni kitovu na mahali pa ziara pa waumini wacha-Mungu na wenye fadhila tele, ambapo kando yake kumechipuka chuo kikuu na kitovu muhimu zaidi cha elimu ya Kiislamu (Hawza ya Kielimu) katika ulimwengu wa Kiislamu. Chuo hicho cha kidini, sambamba na kuendeleza malengo ya kielimu na kidini, kinatambulika vyema kama kiini kikuu cha mapambano, kusimama kidete, na mwamko wa mapinduzi ya Kiislamu.
@@@
Siku kama ya leo miaka 1689 iliyopita, yaani sawa na tarehe 22 Septemba mwaka 337, vilianza vita vya miaka 13 kati ya Iran na Roma katika utawala wa Shapur II (Dhul Aktaf), wa silsila ya watawala wa Sasani na ambavyo katika historia vilifahamika kama vita vya duru ya kwanza. Vita vya duru ya pili vilianza mwaka 359, ambapo katika duru zote, Wairani waliibuka na ushindi. Katika duru ya kwanza ambapo vita hivyo vilidumu hadi mwaka 350, Waroma walipoteza kila kitu walichokuwa wakikidhibiti eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterranean, na mfalme wao aliuawa katika duru ya pili ya vita hivyo.
@@@
Tarehe 10 Rabiuthani mwaka 1330 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 118 iliyopita Haramu tukufu ya Imam Ali bin Mussa Ridhaa, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Mash'had huko kaskazini mwa Iran ilishambuliwa kwa mizinga na wavamizi wa Kirusi.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Mmarekani, Morgan Shuster kuanzisha kikosi maalumu cha polisi ya Hazina Kuu ya Iran.
Urusi iliitambua hatua hiyo kuwa ni kinyume na maslahi yake haramu nchini. Mashambulizi hayo yalisababisha hasara kubwa kwa haramu ya mjukuu huyo wa Mtume (saw) na mali za thamani za eneo hilo tukufu ziliporwa na wavamizi hao.
@@@
Miaka 46 iliyopita, siku ya tarehe 31 Shahrivar mwaka 1359 H.Sh (Septemba 22, 1980)
Kufuatia uvamizi mpana wa vikosi vya anga na vya nchi kavu vya jeshi la utawala wa zamani wa Iraq, uchokozi haramu na wa jumla wa kijeshi wa utawala huo dhidi ya udadhuma wa ardhi ya Iran ulianza rasmi.
Katika siku za mwanzo za uvamizi huo wa Iraq, miji michache na vijiji vya Iran vilitekwa nyara, na mamia ya wanawake na watoto wasio na silaha wa Kiirani waliuawa shahidi kutokana na tamaa ya kutawala ya Saddam. Kwa upande mwingine, madola makubwa ya kimataifa yaliyoona maslahi yao yasiyohalali katika kanda ya Ghuba ya Uajemi yakiwa hatarini kwa kushinda kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, na hivyo waliupa utawala wa Saddam msaada mkubwa wa kifedha, kijeshi, kisiasa, na kipropaganda; lakini hawakufikia lengo lao la kuanguka kwa mfumo mchanga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Sababu ni kwamba vijana wanamapambano wa Kiislamu wenye Imani imara wa Iran walizuia uvamizi huo wa Iraq kwa ushujaa wa kipekee. Hatimaye, jeshi la kivita la utawala dhalimu wa Saddam, baada ya kuvumilia kushindwa mfululizo kutoka vikosi vya jeshi la Iran ya Kiislamu, lilirudishwa nyuma hadi mipaka ya kimataifa inayotambulika, na Agosti 20, 1988, kwa mujibu wa Azimio la 598 la Umoja wa Mataifa, makubaliano ya kusitisha mapigano yalitiwa sahihi na kuanzishwa kati ya nchi mbili.
Katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kila mwaka katika sikukuu ya kumbukumbu ya kuanza kwa uchokozi wa Iraq dhidi ya Iran tarehe 31 Shahrivar 1359 H.Sh, kwa heshima ya kutambua juhudi na damu ya taifa la Waislamu wa Iran waliolinda taifa lao dhidi ya uchokozi huo, hafla maalum za kihistoria zinazodumu kwa muda wa wiki moja zinazinduliwa chini ya jina la “Wiki ya Ulinzi Mtakatifu” (Hafte-ye Defa’ Moqaddas).
@@@
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, nchi ya Mali iliyo kaskazini magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru. Karibu miaka elfu mbili iliyopita nchi ya Mali ilikuwa na utamaduni mkubwa na uliong'ara. Hata hivyo nchi hiyo tangu karne ya 18 hadi ya 19 Miladia ilikuwa moja ya tawala za ufalme wa Sudan. Baada ya Morocco kutwaa baadhi ya maeneo yaliyokuwa chini ya tawala za ufalme wa Sudan ikiwemo Mali, tawala mbalimbali za kikabila nchini Mali zilifanikiwa kuingia madarakani. Satwa ya Wafaransa nchini Mali ilianza mnamo karne ya 19 na hadi kufikia mwaka 1898 nchi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Ufaransa. Hata hivyo Mali ambayo ilikuwa ikiitwa Sudan ya Ufaransa, mwaka 1958 ilianza kujitawala na mwaka 1960 ikajipatia uhuru wake kamili.
@@@
Katika siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, nchi ya Bulgaria ilijipatia uhuru kutoka kwa utawala wa Othmania. Bulgaria ilianza kutawaliwa na utawala huo mwishoni mwa karne ya 14. Wakati huo maudhi dhidi ya Wakristo yalianza na kuendelea kwa karibu miaka 500 ya udhibiti wa Othmania kwenye nchi hiyo na suala hilo liliibua uasi wa mara kwa mara wa raia wa Bulgaria. Hatimaye mwaka 1878 nchi hiyo ilipata uhuru na kujitangazia mamlaka ya ndani. Tarehe 22 Septemba mwaka 1908 mfalme wa wakati huo wa Bulgaria alitangaza uhuru kamili wa nch hiyo.