Sep 20, 2026 04:36 UTC
  • Jumapili, 20 Septemba 2026

Leo ni Jumapili 8 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria mwafaka na 20 Septemba 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1216 iliyopita, yaani tarehe 8 Rabiu-Thani, mwaka 232 Hijria Qamaria alizaliwa katika mji wa Madina, Imamu Hassan al-Askari mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume SAW. Akiwa katika umri wa utotoni, alilazimishwa na makhalifa wa Bani Abbas akiwa na baba yake Imam Hadi AS, kuondoka mji huo na kuhamia Samarra, Iraq ambao wakati huo ulikuwa makao makuu ya utawala wao. Japokuwa mtukufu huyo hakuweza kuishi zaidi ya miaka 28 lakini aliacha nyuma maarifa muhimu na adhimu ya Kiislamu. (Imam Hassan al- Askari alihudumia Uimamu kwa muda wa miaka 6 tu akipitisha sehemu kubwa ya miaka hiyo michache uhamishoni na kwenye jela za Bani Abbas). Sambamba na kukupeni mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa nuru hiyo ya kizazi cha Bwana Mtume SAW nakunukulieni hapa moja ya semi adhimu za Imamu huyo mtukufu isemayo: Mwenye kuchunga zaidi haki za watu, ndiye mwenye daraja ya juu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

***

Katika siku kama ya leo miaka 1091 iliyopita yaani mwaka 357 Hijria, aliaga dunia Abu Firas al-Hamdani malenga na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Mbali na kuandika mashairi, Abu Firas al-Hamdani alikuwa mpiganaji na miongoni mwa watu wa karibu kwa Seif ad-Dawlah mtawala wa Halab na alikuwa miongoni mwa makamanda wake.

***

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30 na kwenda kwa kasi ndogo na lilitengenezwa na Gordon Branz, raia wa Uingereza. Hii leo mabasi bora na ya kisasa ni miongoni mwa vyombo muhimu vya usafiri kote duniani.

***

Miaka 159 iliyopita, katika siku kama ya leo, nchi ya Hungary iliunganishwa na ardhi ya Austria, na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo. Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia. Hungary iko Ulaya ya Kati, ikipakana na Romania, Austria, Jamhuri ya Czech, Slovakia na Yugoslavia. Kwa sasa, Hungary inaongozwa kwa mfumo wa Jamhuri.

***

Tarehe 20 Septemba miaka 47 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Bokasa alizaliwa mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa. Alikuwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa. Bokasa alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake, David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo.  Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

***