Ijumaa Septemba 25 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Ijumaa 13 Rabiul Thani 1448 Hijria Qamaria mwafaka na 25 Septemba 2026 Miladia
Siku kama ya leo miaka 1229 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 219 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham msomi na mwanazuoni mkubwa wa Kiarabu. Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu ya fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw). Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha al Sira al Nabawiyya ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw)..
@@@
Katika siku kama ya leo miaka 129 iliyopita sawa na 25 Septemba 1897 Miladia alizaliwa mwandishi wa Kimarekani kwa jina la William Faulkner. Faulkner hakukamilisha masomo yake ya juu na alianza kujishughulisha na kazi mbalimbali ka ajili ya kuendesha maisha. Mwandishi huyo mashuhuri alianza kuandika hadithi mwaka 1925 baada ya kufahamiana na Sherwood Anderson mwandishi mwenzie wa Kimarekani. Katika hadithi zake Faulkner alikuwa akibainisha hali mbaya ya kijamii huko Marekani hususan ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiwakabili raia weusi wa nchi hiyo. Riwaya za mwandishi huyo zimekuwa na taathira kubwa katika sekta ya uandishi wa sasa nchini Marekani. Mwaka 1950 mwandishi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel.
@@@
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, iliasisiwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Jumuiya hiyo ni ya pili kwa ukubwa baada ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa na nchi wanachama 57 katika mabara zaidi ya manne. Jumuiya hiyo inahesabiwa kuwa sauti ya ulimwengu wa Kiislamu yenye jukumu la kulinda maslahi ya Waislamu, kueneza moyo wa amani na kuratibu masuala ya Waislamu. Jumuiya hiyo iliundwa katika mkutano wa Kihistoria uliofanyika Rabat nchini Morocco tarehe 25 Septemba mwaka 1969 kama jibu la hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa al Aqsa huko Baitul Muqaddas.
@@@
Siku kama ya leo miaka 23, sawa na 25 Septemba 2023 iliyopita aliaga dunia Edward Said, mwandishi na mwanafikra wa Kipalestina kutokana na maradhi ya saratani. Said alizaliwa mwaka 1935 katika familia ya Kikristo. Alielekea Marekani kwa ajili ya kudumisha elimu akiwa na umri wa miaka 17 na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika Chuo kikuu cha Harvard. Kitu kilichompa umashuhuri zaidi Prf. Edward Said katika upeo wa kimataifa ni jitihada zake kubwa za kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina bila ya kusita. Mwanafikra huyo mtajika alifikisha sauti ya kudhulumiwa wananchi wa Palestina katika masikio ya walimwengu kupita makala na vitabu vyake. Ameandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni kile alichokipa jina la Orientalism ambacho ndani yake anaeleza jinsi wataalamu wa masuala ya Mashariki wa Wamagharibi wanavyotumiwa kama wenzo wa wakoloni kwa ajili ya kuhalalisha uporaji wa mali na maliasili za mataifa ya Mashariki mwa dunia.
@@@
Miaka 92 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 3 Mehr mwaka 1313 Hijria Shamsiya
Faqih wa ngazi za juu, Ayatullah Mirza Abolqasem Kabir Qomi, alirejea kwa Mola wake.
Ayatullah Sheikh Abolqasem Kabir Qomi alizaliwa mwaka 1262 Hijria Shamsiya na baada ya kukamilisha hatua za awali na za kati za masomo yake mjini Qom, alipata fursa ya kunufaika pakubwa na hekima na elimu ya ma-Ayatullah wakuu: Mirza Khalil Tehrani Najafi, Akhund Mulla Muhammad Kazim Khorasani, na Sayyid Muhammad Kazim Yazdi mjini Najaf, pamoja na Mirza Muhammad Hassan Ashtiani mjini Tehran.
Shakhsia mashuhuri na viongozi wakubwa wa kidini, kama vile ma-Ayatollah: Imam Khomeini, Sayyid Muhammad-Reza Golpaygani, Akhund Mulla Ali Hamedani, Sayyid Mustafa Safaei Khansari, na makumi ya wanazuoni wengine hodari, ni miongoni mwa wanafunzi walionufaika moja kwa moja na elimu yake.
Hatimaye, Ayatollah Kabir Qomi alifariki dunia tarehe 3 Mehr mwaka 1313 Hijria Shamsiya, sawa na tarehe 15 Jumada al-Thani 1353 Hijria Qamaria, akiwa na umri wa miaka 73, na akazikwa mjini Qom.
@@@
Na Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 3 Mehr, 1321 Hijria Shamsia.
“Muhammad Yusufzadeh,” anayefahamika zaidi kama “Ghamam Hamedani,” mwandishi na mshairi mahiri wa Kiirani, aliaga dunia mjini Hamedan.
Ghamam Hamedani alikuwa na umahiri na elimu ya kina katika nyanja za mantiki, falsafa ya Kiislamu, na fasihi, hususan katika ushairi wa Kifarsi. Mbali na shughuli zake za kifasihi, alikuwa miongoni mwa wapiganaji wa mstari wa mbele katika vuguvugu la Mapinduzi ya Katiba (Mashruteh). Hata hivyo, wakati vuguvugu hilo la Katiba lilipopoteza mwelekeo wake wa awali na vibaraka wa udikteta kujipenyeza katika safu za uongozi wa harakati hizo, Ghamam Hamedani alijiondoa katika medani ya siasa na kuelekeza nguvu zake katika kusambaza mafundisho ya kijamii na shughuli za fasihi.
Kazi pekee iliyobaki ya Ghamam Hamedani ni diwani yake ya mashairi, ambayo hata hivyo, inajumuisha chini ya theluthi moja ya kazi zote alizotunga katika uhai wake.