Alkhamisi, Oktoba Mosi, 2026
Leo ni Alkhamisi mwezi 19 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria sawa na Oktoba Mosi, 2026 Miladia.
Miaka 2348 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe Mosi Oktoba mwaka 322 BC, aliaga dunia mwanafalsafa mashuhuri wa Ugiriki ya kale, Aristotle akiwa na umri wa miaka 62. Aristotle alizaliwa mwaka 384 BC katika mji wa Stagira ambao leo hii ni sehemu ya jimbo la Ugiriki la Macedonia ya Kati. Baba yake alikuwa daktari wa mfalme wa Macedonia, na kwa sababu hiyo alirithi mali nyingi kwa baba yake ambaye aliaga dunia, yeye akiwa angali kijana mdogo. Kwa mtazamo wa mwanafalsafa huyo wa Kigiriki, maisha ya fanaka hupatikana kwa kuwa na uvumilivu, sambamba na kuzingatia msingi wa kiasi na wastani katika ufanyaji mambo; na maisha ya furaha nayo hupatikana kwa kuishi vizuri kunakotokana na kufanya kazi vizuri.
&&&
Tarehe 9 Mehr katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imepewa jina la Siku ya Mshikamano na Watoto na Vijana wa Palestina kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi mtoto mdogo wa Kipalestina Muhammad al-Durrah.
Mnamo mwaka 2000, katika siku kama ya leo, Muhammad al-Durrah mtoto mdogo wa miaka 12 aliuliwa shahidi kinyama na wanajeshi wa utawala wa kizayuni wa Israel. Kijana huyo aliuawa shahidi baada ya askari mdunguaji wa Israel kumlenga kwa lengo la kumuua kwa kumpiga risasi ya kichwa. Tukio hilo lilipelekea vyombo vya habari kuakisi kila kipengele cha mauaji hayo ulimwenguni kote. Kuuawa shahidi Muhammad al-Durrah kulimfanya mtoto mdogo huyo wa Kipalestina kuwa nembo ya Muqawama na Siku ya Watoto Wasio na Hatia wa Palestina. Na kwa mnasaba huo, Bunge la Iran likaipitisha Oktoba Mosi katika kalenda ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa Siku ya Mshikamano na ya Kuwahurumia Watoto na Vijana Chipukizi wa Palestina.
&&&
Miaka 77 iliyopita mwaka 1949 katika siku kama ya leo, ilitangazwa rasmi Jamhuri ya Watu wa China chini ya uongozi wa Mao Zedong.
Nchi ya China yenye ustaarabu mkongwe, ilikuwa chini ya udhibiti wa madola ya Ulaya kuanzia mwishoni mwa karne ya 16. Mara kadhaa Wachina walianzisha vita dhidi ya mkoloni hasa Muingereza ili kuikomboa nchi yao lakini hawakufanikiwa.
Mwaka 1912 mapinduzi yaliyoongozwa na Sun Yat-Sen dhidi ya mfumo wa utawala wa Kifalme yalizaa matunda na kiongozi huyo akachaguliwa kuwa rais wa China.
&&&
Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, yaani ya Oktoba Mosi 1960 nchi ya Nigeria ilipata uhuru.
Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 ardhi ya Nigeria iligeuzwa kuwa moja ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya majeshi ya Uingereza, viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria.
Mwaka 1914 Uingereza iliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ikajitangazia kuwa na utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ikajipatia uhuru katika siku kama ya leo.
&&&
Siku kama ya leo miaka 342 iliyopita yaani Oktoba Mosi 1684 alifariki dunia Pierre Corneille mwandishi na malenga wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 78. Pierre alipenda sana kujifunza uandishi wa tamthiliya na akafanikiwa kusonga mbele katika fani hiyo. Alifahamika kwa lakabu ya baba wa uandishi wa tamthiliya wa Ufaransa na mwasisi wa tamthiliya ya kiwango cha juu yaani (Classic Theatre).
&&&
Na tarehe Mosi Oktoba ni siku ya Wazee Duniani.
Siku hii ilitengwa kwa ajili ya kuwakirimu na kuwaenzi watu wa tabaka hilo.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa hapa nchini Iran na kutokana na mabadiliko yaliyotokea baada ya Mapinduzi ya Kiislamu na utamaduni wa Kiislamu unaotawala hapa nchini wazee na watu wazima wanapewa nafasi ya juu ndani ya familia na katika jamii…/