Oct 04, 2026 03:04 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili 22 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria mwafaka na 04 Oktoba 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1152 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Musa al-Mubarqa' (المبرقع)mtoto wa Imam Muhammad Taqi al-Jawad na ndugu wa Imam Hadi AS aliaga dunia katika mji mtakatifu wa Qum, Iran. Alizaliwa Madina mwaka 214 Hijria na mpaka anafikisha umri wa miaka 6 ambapo baba yake aliuawa shahidi, alikuwa chini ya malezi na usimamizi wa baba yake huyo. Baadaye alijifunza elimu kwa kaka yake, yaani Imam al Hadi AS. Musa al-Mubarqa' kipindi fulani aliishi katika mji wa Kufa katika Iraq ya leo na alipokuwa na umri wa miaka 42 alisafiri na kuelekea katika mji wa Qum, Iran. Aliishi Qum akijishughulisha na ulinganiaji na kueneza dini ya Uislamu hadi alipofariki dunia katika siku kama ya leo. Musa al-Mubarqa' ana daraja ya juu ya kielimu na alikuwa mpokezi wa Hadithi. Aidha alisifika mno kwa taqwa na uchamungu.

***

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, Ubelgiji ilijitangazia uhuru. Mwanzoni mwa karne ya 18 Ubelgiji ilikuwa chini ya udhibiti wa Austria, huku ikidhibitiwa na Ufaransa mwishoni mwa karne hiyo hiyo. Hata hivyo baada ya Napoleon Bonaparte kushindwa na madola ya Ulaya, mwaka 1815 Ubelgiji na Uholanzi ziliunda muungano. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa muda mrefu kufuatia Wabelgiji wa Kikatoliki kuanzisha uasi dhidi ya Waholanzi wa Kiprotestanti na hivyo kuamua kujitangazia uhuru wao katika siku kama ya leo.

***

Katika siku kama ya leo miaka 98 iliyopita tabibu Alexander Fleming alivumbua dawa ya penicillin. Fleming ambaye alikuwa daktari maarufu nchini Uingereza, alizaliwa tarehe Sita Agosti mwaka 1881 katika familia ya wakulima mjini Lochfield farm, magharibi mwa Scotland. Fleming alivumbua dawa hiyo baada ya kuona kuwa askari wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukumbwa na bakteria wa maambukizi kwenye majeraha, suala ambalo lilimtia wasi wasi mkubwa. Miaka 10 baada ya kumalizika vita, sawa na tarehe Nne Oktoba mwaka 1928 Miladia, Fleming alifanikiwa kuvumbua dawa ya penicillin, ambayo huua vijidudu vya maambukizi kwenye kidonda.

***

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita satalaiti ya kwanza ilirushwa angani na msomi wa Urusi ya zamani na kwa utaratibu huo zama za udhibiti wa anga zikawa zimeanza. Satalaiti hiyo iliyopewa jina la Sputniki 1 ilizunguka dunia mara 1400 kwa siku 92 na kwa mara ya kwanza ikafikisha ujumbe wa radio kutoka angani kuelekea ardhini. 

***