Oct 06, 2026 06:58 UTC
  • Jumanne, 06 Oktoba, 2026

Leo ni Jumanne mwezi 24 Mfunguo Saba, Rabiuthani 1448 Hijria, sawa na tarehe 6 Oktoba, 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita yaani tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, vilianza vita vya nne kati ya Waarabu na utawala wa kizayuni wa Israel. Katika siku hiyo jeshi la Misri lilivishambulia vikosi vya utawala huo ghasibu katika oparesheni ya kushtukiza katika upande wa pili wa Mfereji wa Suez. Baada ya kuvunja mstari imara wa ulinzi wa Barlow, vikosi hivyo vikafanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai. Katika vita hivyo, vikosi vya majeshi ya Misri na Syria viliyatia hasara kubwa majeshi ya utawala wa Israel na idadi kadhaa ya ndege za kivita za Wazayuni zilisambaratishwa. Hata hivyo kutokana na hatua ya Marekani ya kuupatia silaha za kisasa utawala huo wa Kizayuni, Waarabu walipoteza baadhi ya ushindi waliokuwa wameupata katika vita hivyo.

&&&

Miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 6 Oktoba 1981, bandari ya Aqaba ya nchini Jordan ilikabidhiwa kwa Iraq ili kuitumia kilojistiki kwa ajili ya vita dhidi ya Iran. Kufuatia kuanza vita vamizi vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Hussein wa Jordan, alitangaza kumuunga mkono kikamilifu Saddam Hussein wakati wa ziara ya masaa 24 aliyofanya nchini Iraq. Akiwa katika ziara hiyo, mfalme huyo wa Jordan wa wakati huo alisema: "Nchi za Kiarabu ni kitu kimoja na zina hatima moja, na kwa hivyo lazima ziungane katika kuiunga mkono Iraq." Kufuatia ziara hiyo, Waziri Mkuu wa Jordan aliamuru vyombo vyote vya usafirishaji vya nchi hiyo vitumiwe kusafirishia chakula na vifaa vya kijeshi na vya raia kuelekea Iraq. Kwa kuanza rasmi vita vya Iraq dhidi ya Iran mnamo Septemba 22, 1980 na kuvurugika usalama katika eneo la Arvand Rud, serikali ya Jordan iliipatia Iraq bandari ya Aqaba iliyoko katika Bahari Nyekundu ili misaada ya kijeshi ya kigeni ihamishiwe Iraq kutokea kwenye bandari hiyo. Kwa upande mwingine, sambamba na kuanza vita, Mfalme Hussein alitoa amri ya kupelekwa wanajeshi elfu arubaini wa nchi yake kwenye mpaka wa Iraq ili itakapolazimu waweze kuingia haraka nchini humo kuusaidia utawala wa Baathi wa nchi hiyo.

&&&

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Oktoba 6, 1981 maafisa kadhaa wa jeshi waliokuwa wanachama wa harakati ya Kiislamu la "Al-Jihad" au Jihaduli-Islami ya Misri walimshambulia kwa risasi na kumuua rais wa wakati huo wa Misri, Muhammad Anwar Sadat. Rais huyo aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano ya udhalilishaji ya Camp David mnamo mwaka 1978 na utawala ghasibu wa Israel sambamba na kuutambua rasmi utawala huo haramu. Kwa hatua yake hiyo, Saadat alihesabiwa kuwa msaliti wa malengo matukufu ya Waislamu na Waarabu. Kwa upande mwingine hatua hiyo ilipelekea kutengwa Misri na nchi za Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo ndipo makundi ya Kiislamu na wanamapambano wa Misri wakaamua kumuua Saadat, ambaye alionekana kama msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala huo ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, mmoja wa maafisa wa jeshi la Misri wakati huo. 

&&&

Na leo tarehe 6 Oktoba, Misri, ambayo ni moja kati ya tamaduni za kale zaidi duniani ilianzisha serikali ya jamhuri yenye bunge baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Jamhuri ya Kiarabu ya Misri ina siku mbili za taifa ambazo ni tarehe 23 Julai na 6 Oktoba. Tarehe 23 Julai ni siku ya mapinduzi yaliyouangusha utawala wa kifalme wa Mfalme Faruq hapo mwaka 1952 mapinduzi ambayo yaliandaa uwanja wa kutangazwa jamhuri ya nchi hiyo…/