Hukumu za Ibada ya Hija- Ihram
Baada ya miaka mingi na kuwa mbali na Makka, Mtume Muhammad (saw) na Masahaba wake walielekea katika eneo hilo kwa ajili ya kufanya ibada ya Umra katika mwaka wa 6 wa Hijria. Wote walivaa Ihram mahali paitwapo Dhul-Hulaifah (Msikiti Shajara), ambapo palikuwa umbali wa kilomita 450 kutoka Makka.
Ihram ni moja ya nguzo za ibada ya Hija na Umrah, na mtu aliye katika Ihram anaitwa Muhrim, na anapaswa kufuata kanuni makhsusi. Muhrim haruhusiwi kufanya baadhi ya mambo yaliyokuwa halali kwake kabla ya kuvaa vazi la Ihram. Mojawapo ya mambo hayo ni kuwinda wanyama wa jangwani, iwe wanyama wanaolisha au ndege. Kuuwa mnyama au kula nyama yake, hata kama amewindwa na asiyekuwa Muhrim, huifanya nyama hiyo kuwa na hukumu ya mzoga, na huwa haramu kuila. Mtu aliyevaa vazi la Ihram haruhusiwi hata kumwongoza muwindaji kwa ajili ya kukamata kiwindwa, au kuzuia njia ya mnyama anayewindwa. Ni haramu kwa Muhrim kula hata mayayi ya ndege wa nyandani.
Mtume (SAW) na Waislamu waliokuwa pamoja naye walielekea Makka baada ya kuhirimu katika Msikiti wa Shajara. Njiani, walikutana na wanyama pori wengi. Wanyama hao walikuwa karibu yao sana kiasi kwamba, Waislamu wangeweza kuwakamata kwa kuwapiga mkuki au hata kwa mikono yao, lakini walijizuia ili kutii sheria ya Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, miongoni mwao walikuwepo baadhi waliotaka kuwawinda wanyama hao na kufaidika na nyama zao. Wakati huu, iliteremshwa Aya ya 94 ya Suratul Maidah na kuwaonya watu kama hao kwamba, Mwenyezi Mungu anakujaribuni kwa mambo haya madogo ili apate kujua ni kwa kiasi gani mnafuata na kutii amri Zake. Aya hiyo inasema:
يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَيَبۡلُوَنَّكُمُ ٱللَّهُ بِشَيۡءٖ مِّنَ ٱلصَّيۡدِ تَنَالُهُۥٓ أَيۡدِيكُمۡ وَرِمَاحُكُمۡ لِيَعۡلَمَ ٱللَّهُ مَن يَخَافُهُۥ بِٱلۡغَيۡبِۚ فَمَنِ ٱعۡتَدَىٰ بَعۡدَ ذَٰلِكَ فَلَهُۥ عَذَابٌ أَلِيمٞ
Enyi mlioamini! Hakika Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa wanyama wa kuwinda inayowafikia mikono yenu na mikuki yenu, ili Mwenyezi Mungu amjue nani anayemuogopa kwa ghaibu. Basi atakayeruka mipaka baada ya hayo atapata adhabu iumizayo.
Miongoni mwa nukta muhimu za kuashiriwa kuhusiana na Aya hii ni kwamba, wakati wowote Mwenyezi Mungu anapomkataza mtu kufanya jambo fulani, huimarisha uwezo wake. Kwa mfano, wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, tunajizuia kula, kunywa na kadhalika na kidhahiri, nguvu zetu za mwili hupungua; lakini kinyume chake, subira, uvumilivu na nguvu zetu za kiroho huimarika zaidi. Vivyo hivyo wakati wa ibada ya Hija; tunapokatazwa kuwinda, tunapata uwezo wa kudhibiti matakwa na matamanio ya nafsi zetu.
Nukta nyingine muhimu katika Aya hii ni suala la kulinda mazingira, kwa sababu iwapo uwindaji ungehalalishwa kwa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, kizazi cha wanyama wengi kingetoweka na kuangamia katika eneo hilo ambalo lina wanyama wachache kutokana na ukame, kwa kuzingatia idadi kubwa ya mahujaji wanaokwenda katika ardhi hiyo takatifu kila mwaka.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuharamisha kuwinda wanyama pori kwa mahujaji walio katika Ihram, baadhi ya Waislamu walikwenda kwa Mtume (saw) na kuuliza maswali kuhusu jinsi ya kutayarisha chakula kinachohitajiwa na mahujaji. Walisema, ikiwa hatuwinda wakati wa Hija, basi tutumie chakula gani? Wakati huu ndipo ilipoteremshwa Aya ya 96 ya Suratul Maidah na kuruhusu kuwinda na kula wanyama wa baharini. Aya hiyo inasema:
أُحِلَّ لَكُمۡ صَيۡدُ ٱلۡبَحۡرِ وَطَعَامُهُۥ مَتَٰعٗا لَّكُمۡ وَلِلسَّيَّارَةِۖ وَحُرِّمَ عَلَيۡكُمۡ صَيۡدُ ٱلۡبَرِّ مَا دُمۡتُمۡ حُرُمٗاۗ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ ٱلَّذِيٓ إِلَيۡهِ تُحۡشَرُونَ
Mmehalalishiwa kuvua vya baharini na kuvila, kwa manufaa yenu na kwa wasafiri. Na mmeharimishiwa kuwinda wanyama wa bara maadamu mko katika Ihram. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa.
Ilikuwa wakati wa ibada ya Hija na Waislamu walikuwa wamekusanyika kandokando ya Mtume (saw) wakisikiliza maneno yake kuhusu matendo na hukumu za Hija. Mtume (saw) alikuwa bado hajamaliza maneno yake pale mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ukasha ambaye alikuwa mzungumzaji sana, alipomuuliza: Ya Rasullah! Je, amri hii ni ya milele na tunatakiwa kuhiji kila mwaka? Mtume (saw) hakujibu swali lake kutokana na maslahi fulani. Ukasha aliuliza tena swali hilo hilo, lakini Mtume alinyamaza kimya. Kwa mara ya tatu Ukasha alirudia swali lake kwa ufidhuli.
Mtume (saw) alipoona ukaidi wake alivunja ukimya na kumkemea kisha akasema: Ole wako! Mbona unang'ang'ania swali hilo? Nikisema: Ndiyo! Hija itakuwa wajibu kwako kila mwaka! Katika hali hii, itakuwa juu ya uwezo wako na hutaweza kuitekeleza. Wakati huo huo, iwapo utapinga na usiitekeleze, utakuwa umepinga hukumu ya Mtume wako, na utakuwa mwenye dhambi mbele ya Mungu. Sasa, kwa kuwa nimekaa kimya na sijakwambia chochote, hupaswi kufuatilia. Elewa kuwa kusemasema sana na ukaidi viliziangamiza baadhi ya kaumu zilizopita.
Baada ya hapo, Mtume (saw) alimwambia Ukasha na waliokuwa karibu yake kwamba: Tekelezeni amri zote ninazokupeni kadiri ya uwezo wenu, na jizuieni kufanya chochote ninachokukatazeni. Hapa ndipo zilipoteremshwa Aya za 101 na 102 za Suratul Maidah zikiwakataza Waislamu kuuliza maswali kifidhuli.
يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَا تَسۡـَٔلُواْ عَنۡ أَشۡيَآءَ إِن تُبۡدَ لَكُمۡ تَسُؤۡكُمۡ وَإِن تَسۡـَٔلُواْ عَنۡهَا حِينَ يُنَزَّلُ ٱلۡقُرۡءَانُ تُبۡدَ لَكُمۡ عَفَا ٱللَّهُ عَنۡهَاۗ وَٱللَّهُ غَفُورٌ حَلِيمٞ. قَدۡ سَأَلَهَا قَوۡمٞ مِّن قَبۡلِكُمۡ ثُمَّ أَصۡبَحُواْ بِهَا كَٰفِرِينَ
Enyi mlioamini! Msiulize mambo ambayo mkidhihirishiwa yatawachukiza. Na mkiyauliza inapoteremshwa Qur'ani mtabainishiwa. Mwenyezi Mungu amesamehe hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mpole. Waliyauliza watu wa kabla yenu, kisha wakawa wenye kuyakataa.
Inatupasa kuweka wazi kwamba, Aya hizi hazikatazi watu kuuliza maswali na kutafuta elimu, kalla wa hasha. Kwa sababu Qur'ani inawaamuru Waislamu kuuliza na kutafuta ujuzi na elimu. Hivyo basi, inaeleweka kuwa, maana ya Aya hizi ni kuuliza maswali pasipo mahali pake, kwa ajili ya ubishi, ukaidi na kutafuta visingizio, ambavyo mara nyingi huchanganya akili za watu, kumsumbua mzungumzaji, na kuparaganyisha hotuba na malengo yake.