Kwa nini ushawishi wa Kizayuni nchini Marekani hauna tena taathira kama zamani?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140578-kwa_nini_ushawishi_wa_kizayuni_nchini_marekani_hauna_tena_taathira_kama_zamani
Ushindi wa Abdul El-Sayed katika uchaguzi wa mchujo wa Chama cha Democratic jimboni Michigan umeashiria kushindwa wazi kwa mara ya kwanza kwa fikra inayosema kwamba pesa, ushawishi na kampeni hasi huamua matokeo ya kisiasa ya moja kwa moja nchini Marekani.
(last modified 2026-08-11T07:03:01+00:00 )
Aug 11, 2026 06:16 UTC
  • Kwa nini ushawishi wa Kizayuni nchini Marekani hauna tena taathira kama zamani?

Ushindi wa Abdul El-Sayed katika uchaguzi wa mchujo wa Chama cha Democratic jimboni Michigan umeashiria kushindwa wazi kwa mara ya kwanza kwa fikra inayosema kwamba pesa, ushawishi na kampeni hasi huamua matokeo ya kisiasa ya moja kwa moja nchini Marekani.

Kidhahiri, kinyang'anyiro cha mchujo cha kiti cha Seneti cha Chama cha Democratic jimboni Michigan kilionekana kuwa moja tu ya mashindano mengi ya ndani ya vyama kabla ya kufanyika uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani. Ama kwa hakika mchuano huo ulikuwa uwanja wa mapambano ya kupimana nguvu kati ya mrengo wa siasa za jadi wa Marekani na harakati inayoibuka ya maendeleo.

Matokeo ya kinyang'anyiro hicho yamevuka mipaka ya kuchagua mgombea wa chama tu na kutoa ujumbe kuhusu mabadiliko yanayotokea taratibu katika maoni ya umma nchini Marekani, hasa kuhusiana na mauaji ya umati ya Gaza, ushawishi wa lobi za kisiasa na mustakabali wa Chama cha Democratic.

Abdul El-Sayed, daktari na afisa wa zamani wa afya ya umma, amefanikiwa kumshinda Haley Stevens, mtu anayeungwa mkono na sehemu kubwa ya viongozi wa jadi wa Chama cha Democratic, licha ya mpinzani wake huyo kunufaika na uungwaji mkono mkubwa wa kifedha na kisiasa. Makundi yaliyo karibu na lobi za ushawishi zinazoiunga mkono Israel, hasa AIPAC, yalitumia makumi ya mamilioni ya dola katika jitihada za kuzuia ushindi wake. Sambamba na uungwaji mkono huo wa kifedha, watu wengi mashuhuri ndani ya Chama cha Democratic pia walimuunga mkono Stevens. Hata hivyo, matokeo ya mwisho yalionyesha kuwa ukubwa wa matumizi ya fedha katika kampeni za uchaguzi haudhamini tena ushindi.

Kinachofanya uchaguzi huu kuwa tukio la kihistoria na la mabadiliko makubwa si tu ni kushindwa kwa mgombea au kufeli kwa kundi la ushawishi, bali ni kuibuka kwa mabadiliko makubwa katika mwenendo wa kisiasa katika jamii ya Marekani. Baada ya takriban miaka mitatu ya vita huko Gaza, suala la uungaji mkono usio na masharti wa Washington kwa Tel Aviv limebadilika kutoka kuwa suala la sera ya kigeni na kuwa suala la ndani ya Marekani. Kizazi cha vijana, wapiga kura wenye msimamo wa maendeleo, sehemu kubwa ya Waislamu wa Marekani na Wamarekani wenye asili ya Kiarabu na hata makundi huru ya wapiga kura, sasa wanazingatia sera za serikali ya Marekani kuhusu Mashariki ya Kati wanapowatathmini wagombea wa uchaguzi.

Katika muktadha huu, jimbo la Michigan lina nafasi ya kipekee. Jimbo hili linachukuliwa kuwa mojawapo ya nyanja muhimu zaidi za ushindani wa kisiasa nchini Marekani, na ni makazi ya idadi kubwa zaidi ya Wamarekani wenye asili ya Kiarabu pamoja na mojawapo ya jamii kubwa zaidi za Waislamu nchini humo. Muundo huu wa kijamii ulifanya vita vya Gaza na sera ya Marekani kuhusu utawala wa Kizayuni kuwa masuala muhimu katika kinyang'anyiro hicho, jambo linaloashiria mabadiliko muhimu ikilinganishwa na chaguzi nyingi zilizopita. Wapiga kura katika jimbo hili hawakujikita tu katika masuala ya uchumi, kodi au bima ya afya, bali pia walipiga kura kwa kuzingatia mwelekeo wa kimaadili na kisiasa wa Marekani.

Jambo muhimu zaidi lilikuwa kutofanikiwa kwa kiasi kikubwa mkakati wa kawaida uliotumiwa na makundi ya ushawishi wa kisiasa. Kwa miongo kadhaa, AIPAC limekuwa kundi kubwa zaidi la ushawishi la Kizayuni katika chaguzi za Marekani, likitumia kwa mafanikio uwekezaji mkubwa wa kifedha katika kuwaondoa katika ulingo wa kisiasa wakosoaji wengi wa sera za utawala wa Kizayuni. Gazeti la Haaretz liliripoti kwamba jumla ya matumizi ya kumuunga mkono Stevens yalifikia takriban dola milioni 60, huku zaidi ya dola milioni 30 kati ya kiasi hicho zikitolewa na AIPAC. Gazeti hilo lilielezea pambano la Michigan kama uchaguzi mkuu wenye gharama kubwa zaidi katika historia ya Marekani.

Hata hivyo, kura ya mchujo ya chama cha Democratic cha Michigan imeonyesha kwamba wakati maoni ya umma yanapobadilika, ongezeko la fedha za kampeni si lazima lifanikiwe bali linaweza hata kuwa na madhara. Wapiga kura wanapogundua kuwa rasilimali za fedha za nje zinaongoza matokeo ya uchaguzi, upinzani huongezeka, jambo linalothibitshwa na wachambuzi wengi wa Marekani.

Majibu makali ya Donald Trump kwa ushindi wa El-Sayed pia yanaweza kutathminiwa katika mtazamo huo. Matumizi ya lebo za matusi kama "mkomunisti" au kuwatuhumu wakosoaji wa sera za kigaidi na kibaguzi za utawala wa Kizayuni kuwa na chuki dhidi ya Mayahudi, yamekuwa sehemu ya mjadala wa kisiasa nchini Marekani kwa muda mrefu. Hata hivyo, kuendelea kutumika kwa lugha ya namna hiyo kunazidi kuashiria ugumu wa kutetea hali iliyopo. Tasnia ya siasa ya Marekani si ya upande mmoja tena, na mgawanyiko kuhusu sera ya Mashariki ya Kati sasa umeenea hadi ndani ya vyama vyote viwili vikuu.

Wakati huo huo, ushindi wa El-Sayed unapaswa kutazamwa kama sehemu ya mwelekeo uliojitokeza katika miaka ya hivi karibuni kufuatia kuibuka kwa watu wenye misimamo ya maendeleo ndani ya Chama cha Democratic. Harakati hii inalenga kubadilisha vipaumbele vya sera za Marekani kutoka uingiliaji wa kigeni kuelekea masuala ya ndani, na kutoka ongezeko la bajeti ya kijeshi kuelekea kuwekeza katika huduma za afya, elimu na miundombinu. Ushindi wa Abdul El-Sayed, bila kujali matokeo ya uchaguzi wa mwisho mwezi Novemba, unaonyesha kuwa mtazamo huu si sauti ya mjadala wa pembeni tena, bali ni sehemu ya mapambano makali ya kuwania madaraka nchini Marekani.