Wanajeshi wasiopungua 10 wauawa katika shambulio katikati mwa Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140542-wanajeshi_wasiopungua_10_wauawa_katika_shambulio_katikati_mwa_mali
Wanajeshi wasiopungua 10 waliuawa jana Jumapili katika shambulio lililofanywa katika kambi ya jeshi katikati mwa Mali. Kundi moja la kigaidi lenye mfungamano na mtandano wa al Qaida limedai kuhusika na hujuma hiyo.
(last modified 2026-08-10T03:32:12+00:00 )
Aug 10, 2026 03:09 UTC
  • Wanajeshi wasiopungua 10 wauawa Mali
    Wanajeshi wasiopungua 10 wauawa Mali

Wanajeshi wasiopungua 10 waliuawa jana Jumapili katika shambulio lililofanywa katika kambi ya jeshi katikati mwa Mali. Kundi moja la kigaidi lenye mfungamano na mtandano wa al Qaida limedai kuhusika na hujuma hiyo.

Kambi hiyo, inayopatikana katika kijiji cha San, "ilitekwa kwa muda na wanamgambo wenye silaha.

Wakazi wa eneo hilo wameeleza kuwa mapigano makali yalijiri jana alfajiri.

"Naweza kuthibitisha kuwa lilikuwa shambulio la kigaidi. Tulisikia milipuko mikubwa na milio ya risasi mfululizo; na sasa hali ya utulivu imerejea," ameeleza mkazi mmoja wa kijiji cha San, ambaye hakutaka kutajwa jina.

Jeshi la Mali kwa upande wake limeeleza kuwa kuwa askari wake walichukua "hatua madhubuti ya kujibu mashambulizi dhidi ya kambi hiyo ya jeshi na kwamba" na sasa hali ya mambo imedhibitiwa.

Mali kwa muda sasa inakabiliwa na tishio la makundi ya wanamgambo wenye silaha wakiwemo waasi wa Kituareg wa kaskazini mwa nchi hiyo.

Mali inaongozwa na Meja Jenerali Assimi Goita aliyeingia mamlakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2020.