Mali yataka Afrika ijitegemee katika teknolojia za usalama
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, ametoa wito kwa nchi za Afrika kujenga uwezo wa kujitegemea katika teknolojia za ulinzi na usalama, badala ya kutegemea vifaa na teknolojia kutoka mataifa ya kigeni.
Diop ametoa kauli hiyo katika Mkutano wa Kimataifa wa Usalama Barani Afrika uliofanyika mjini Kigali, Rwanda, akisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuwa na uwezo wa kutengeneza na kuendeleza teknolojia zao za usalama.
Amesema maendeleo ya haraka katika teknolojia kama Akili Mnemba, ndege zisizo na rubani na mifumo ya kijeshi inayojiendesha yanahitaji Afrika kuimarisha uwezo wake wa kiteknolojia na kujenga uhuru katika masuala ya ulinzi na usalama.
Waziri huyo amesema uzoefu wa Mali katika kukabiliana na makundi yenye silaha umeonyesha hatari za kutegemea mataifa ya kigeni katika masuala muhimu ya ulinzi.
Aidha, Abdoulaye Diop amezitaka nchi za Afrika kuacha kuwa watumiaji tu wa vifaa vya kijeshi kutoka nje na badala yake kuwekeza katika utafiti, ubunifu na utengenezaji wa teknolojia za ulinzi ndani ya bara hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, amependekeza kuundwa kwa mifumo ya kikanda ya kukabiliana na vitisho vinavyovuka mipaka, akitoa mfano wa Muungano wa Nchi za Sahel, unaojumuisha Mali, Niger na Burkina Faso.
Diop amezitaka nchi za Afrika kuacha kutegemea vifaa vya kijeshi vinavyotengenezwa na mataifa ya kigeni na kuelekea katika kujitegemea kwa kubuni na kutengeneza teknolojia zao za ulinzi.
Mkutano wa Kimataifa wa Usalama Barani Afrika ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, ukihudhuriwa na zaidi ya wajumbe 300 kutoka nchi 50.
Katika mkutano huo, masuala mbalimbali yalijadiliwa, yakiwemo ongezeko la matumizi ya mifumo ya kijeshi inayojiendesha na teknolojia ya akili bandia, pamoja na athari zake kwa usalama na ulinzi barani Afrika.