Magaidi 70 waangamizwa katika operesheni za jeshi nchini Mali
Jeshi la Mali lilitangaza jana Jumapili kwamba, magaidi wasiopungua 70 waliuawa katika operesheni mbili za kiusalama kaskazini na katikati mwa nchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, operesheni ya kwanza ilifanyika Julai 15 kwa uratibu wa vikosi vya anga kutoka Muungano wa Nchi za Sahel, na kupelekea kuangamizwa karibu magaidi 40 katika eneo la Anderamboukan, kaskazini mwa nchi hiyo.
Operesheni ya pili iliyofanywa siku mbili baadaye na wanajeshi wa Mali, ilisababisha uharibifu wa kambi ya vifaa na mafunzo ya kigaidi katika eneo la Niono katikati mwa Mali, na vifo vya magaidi wapatao 30, taarifa hiyo imeongeza.
Taarifa zinasema kuwa, mbali na magaidi wasiopungua 70 kuuwa katika operesheni hizo, lakini jeshi la Mali limefanikiwa pia kunasa idadi kubwa ya silaha, risasi, pikipiki na magari katika operesheni hizo.
Mapema mwezi huu, magaidi wengine zaidi ya 80 waliuawa katika mashambulizi ya jeshi la Mali yaliyolenga maeneo kadhaa ya katikati na magharibi mwa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Souleymane Dembele, Mkuu wa Kurugenzi ya Habari na Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Mali alieleza kuwa: "Maadui wa amani awali waliwashambulia raia na kisha kutekeleza mashambuliz dhidi ya maeneo kadhaa vikosi vya ulinzi na usalama.
Amesema, maadui wamekuwa wakipata kipigo na hasara kubwa kila mara wanapojaribu kuanzisha mashambulizi dhidi ya jeshi la Mali.