Benin: Askari wetu waliouawa katika shambulio la karibuni ni 54
(last modified Thu, 24 Apr 2025 10:37:17 GMT )
Apr 24, 2025 10:37 UTC
  • Benin: Askari wetu waliouawa katika shambulio la karibuni ni 54

Msemaji wa serikali ya Benin, Wilfried Leandre Houngbedji amesema idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo waliouawa katika shambulio la kigaidi lililotokea kaskazini mwa nchi mnamo Aprili 17 ni 54.

Houngbedji sanjari na kukanusha vikali uvumi ulioenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba askari waliouawa ni zaidi ya 100, pia ametoa rambirambi na mkono wa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo na watu wa Benin kwa ujumla, chombo rasmi cha habari cha Benin cha La Nation kilitangaza hayo jana Jumatano.

Huku akiashiria ukosefu wa ushirikiano kati ya nchi jirani ili kukabiliana na ugaidi kwa njia ya pamoja, Msemaji wa serikali ya Benin amesisitizia umuhimu wa nchi za eneo kuimarisha rasilimali na nyenzo za kiufundi ili kuondoa tishio la ugaidi katika ukanda huo.

Kundi la kigaidi la Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda lilitangaza kuwa wapiganaji wake wamewaua wanajeshi 70 katika shambulizi hilo la Aprili 17 dhidi ya vituo viwili vya kijeshi kaskazini mwa Benin.

Kadhalika shirika la ujasusi la SITE lilisema idadi ya askari waliouawa ni 70 na kuongeza kuwa: Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya mauaji ya askari kwa mkupuo, yaliyofanywa na magaidi wa JNIM nchini humo, katika muda wa muongo mmoja wa shughuli zake katika eneo la Afrika Magharibi.

Taifa hilo la Afrika Magharibi na jirani yake wa pwani ya Togo yamekumbwa na wimbi la mashambulizi ya kigaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Mashambulizi haya yanafanyika huku makundi yenye uhusiano na ISIS na al-Qaeda yakiendelea kupanua satua na uwepo wao katika eneo la Sahel kuelekea kaskazini mwa bara Afrika.