Rais wa Afrika Kusini: Kutohudhuria Marekani mkutano wa G20 ni hasara kwake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133118-rais_wa_afrika_kusini_kutohudhuria_marekani_mkutano_wa_g20_ni_hasara_kwake
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa, kitisho cha Rais wa Marekani Donald Trump kwamba maafisa wa nchi yake hawatahudhuria mkutano wa G20 mjini Johannesburg ni hasara kwa Wamarekani.
(last modified 2025-11-13T07:18:38+00:00 )
Nov 13, 2025 07:18 UTC
  • Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini
    Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa, kitisho cha Rais wa Marekani Donald Trump kwamba maafisa wa nchi yake hawatahudhuria mkutano wa G20 mjini Johannesburg ni hasara kwa Wamarekani.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameeleza kuwa, kususia Marekani kuhudhuria mkutano wa kilele wa G20 nchini Afrika Kusini baadaye mwezi huu hakutazuia kufanyika mkutano wa mataifa hayo makubwa kiuchumi duniani.

"Tutafanya maamuzi ya kimsingi na kutokuwepo kwa Marekani ni hasara kwao," Ramaphosa alisisitiza. "Washington inakwepa jukumu muhimu sana inalopaswa kuchukua kama uchumi mkubwa zaidi duniani."

Rais wa Marekani ametangaza kuwa, hakuna maafisa wa Marekani watakaohudhuria mkutano wa kila mwaka wa Kundi la G20 huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Matamshi haya, yanayotokana na madai yaliyokanushwa ya "mauaji ya halaiki ya wazungu" nchini Afrika Kusini, ni kifuniko tu cha nia halisi ya Trump ya kuiadhibu Afrika Kusini kwa kuishitaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa mauaji ya kimbari huko Gaza.

Trump amekuwa akiendesha kampeni ya kimfumo dhidi ya Afrika Kusini tangu arejee Ikulu ya Marekani Januari 2025. Mnamo Februari mwaka huu, alitoa amri ya utendaji ya kukata misaada yote ya Marekani kwa Pretoria na kukubali wakulima 59 wa Kiafrikana nchini Marekani kama "wakimbizi."

Kususia mkutano wa kilele wa G20, ambao Afrika Kusini ni mwenyekiti wake  kuanzia Desemba 2024, ni sehemu ya mashinikizo ya Marekani dhidi ya Afrika Kusini kutokana nah atua yake ya kuishtaki Israel katika Mahakama ya ICJ.