Iran yasema Lango-Bahari La Hormuz liko wazi kwa Kenya
-
Balozi wa Iran nchini Kenya Dr. Ali Gholampour
Balozi wa Iran nchini Kenya, Dkt. Ali Gholampour, amesema kuwa Lango-Bahari la Hormuz liko wazi kwa Kenya pamoja na mataifa mengine rafiki.
Katika mahojiano na Kenya Times, Balozi Gholampour amezungumzia chanzo cha vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, athari zake kwa binadamu na uchumi, pamoja na mazingira ya kidiplomasia yanayozidi kuwa magumu ambayo Kenya sasa inalazimika kuyapitia katika mahusiano ya kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Gholampour aliweka bayana mtazamo wa Tehran kuhusu namna mzozo huo ulivyoshadidi. Amesema kuwa hali hiyo haikutokea ghafla, bali ni matokeo ya miongo kadhaa ya mvutano wa kisiasa na kiusalama katika eneo hilo.
Pia ametetea hatua za Iran kulipiza kisasi dhidi ya ngome za Marekani na Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia akisema kuwa ni hatua za kujilinda zinazotambuliwa na sheria za kimataifa. Wakati huohuo, amepinga madai kwamba Iran ndiyo inayosababisha misukosuko katika uchumi wa dunia.
Sehemu kubwa ya mahojiano hayo ilijikita katika Lango Bahari la Hormuz — njia muhimu sana ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta- ambayo kwa sasa imeathiriwa kwa kiasi kikubwa. Kwa kuwa Kenya tayari inaathirika kupitia kupanda kwa bei ya mafuta na hatari ya mfumuko wa bei, Balozi Gholampour aliulizwa moja kwa moja kwa nini nchi zisizoegemea upande wowote zinapaswa kubeba gharama za mgogoro ambao hazikuuanzisha.
Amesisitiza kwamba Kenya, kama nchi rafiki, inaweza kutumia Lango-Bahari la Hormuz kwa kufuata taratibu zilizopo kwa sasa, akiongeza kuwa mzingiro wa Marekani katika eneo hilo unazuia uhuru wa usafirishaji baharini.
Mahojiano hayo pia yaligusia uhusiano kati ya Kenya na Iran, ambao umepata changamoto kufuatia kauli za baadhi ya maafisa wa Kenya za kulaani mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Iran dhidi baadhi ya ngome za kijeshi na kiuchumi za Marekani na Israel katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi.
Balozi Gholampour amesisitiza kwamba Kenya bado ni mshirika muhimu kwa Iran, licha ya kwamba mvutano wa sasa umeleta mtikisiko katika uhusiano huo.