Mazungumzo ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Kenya
-
Seyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na Musalia Mudavadi, Waziri Kiongozi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo na mwenzake wa Kenya kuhusu masuala muhimu ya uhusiano wa pande mbili.
Kwa mujibu wa shirika la habari IRNA, Seyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na Musalia Mudavadi, Waziri Kiongozi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, walifanya mazungumzo kwa njia ya simu Jumatano.
Taarifa hiyo imedokeza kuwa, katika mazungumzo hayo, pande mbili walijadiliana kuhusu hali ya hivi karibuni ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ameashiria hali ya kutokuwa na usalama iliyolazimishwa katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango‑Bahari la Hormuz kutokana na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran. Amesisitiza haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti za kimataifa ili kulinda Hati ya Umoja wa Mataifa na kuiwajibisha Marekani kwa kukaidi sheria na makosa yaliyofanywa.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, amesisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa ardhi wa mataifa pamoja na kujiepusha na matumizi ya nguvu. Aidha amesisitiza umuhimu wa diplomasia katika kuleta amani katika eneo.
Mazungumzo hayo yamejiri siku chache baada ya Balozi wa Iran nchini Kenya, Dkt. Ali Gholampour, kusema kuwa Lango-Bahari la Hormuz liko wazi kwa Kenya.. Katika mahojiano na Kenya Times alisisitiza kwamba Kenya, kama nchi rafiki, inaweza kutumia Lango-Bahari la Hormuz kwa kufuata taratibu zilizopo kwa sasa, akiongeza kuwa mzingiro wa Marekani katika eneo hilo unazuia uhuru wa usafirishaji baharini.