Mwanzo wa mpasuko wa kimkakati kati ya pande mbili za Atlantiki
-
José Manuel Albares Bueno,Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania
José Manuel Albares Bueno,Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania, akisisitiza tena sera ya serikali ya nchi yake katika kupinga uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema: 'Marekani haiwezi kutumia vituo vyetu vya anga kwa ajili ya vita dhidi ya Iran.
Matamshi hayo thabiti ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania katika mahojiano na jarida Politico ni ishara ya mabadiliko makubwa katika uhusiano wa pande mbili za Atlantiki. Madrid, kwa kuzuia ndege za kijeshi za Marekani kutumia vituo vyake vya kimkakati vya Morón na Rota na kwa kufunga anga yake dhidi ya operesheni yoyote ya uvamizi dhidi ya Iran, kwa hakika imeweka mstari wake mwekundu. Kwa msingi huu, hakuna kituo chochote nchini Uhispania kitakachokabidhiwa ashington kwa ajili ya vita ambavyo havina uhalali wa kisheria, mashauriano ndani ya NATO na wala kufuata hati ya Umoja wa Mataifa.
Manuel Álbares sabamba na kusisitiza kwamba, Uhispania katika karne ya kumi na nane ilituma majeshi kusaidia uhuru wa Marekani, aliongeza kuwa urafiki wa kihistoria kamwe haumaanishi kupuuza kanuni na sheria za kimataifa, na kwamba Uhispania haitainama au kupiga magoti mbele ya vitisho vya Marekani kuanzia vikwazo vya kibiashara na kuondoa majeshi hadi kusimamishwa uanachama wa NATO. Katika kujibu hilo, Trump, ametaja mwenendo wa Uhispania kuwa 'wa kutisha sana' na kudai kwamba 'hatuna uhusiano wowote na Uhispania', lakini Madrid imesisitiza kwamba matumizi ya vituo hivyo ni kwa mujibu wa mkataba unaolazimisha kuheshimu sheria za kimataifa."
Ukweli wa mambo ni kuwa, Uhispania haiko peke yake katika mkondo huu, bali kuna sauti zinazofanana na hiyo zinazosikika kutoka katikati ya bara Ulaya. Robert Habeck, Naibu Kansela wa Ujerumani, pia katika kujibu vitisho vya kijeshi dhidi ya Iran, sanjari na kuashiria kituo cha anga cha Ramstein ambacho ni moja ya vituo muhimu zaidi vya vifaa na suhula za kijeshi za Marekani barani Ulaya, ameonya kwamba: 'Kuwa na ushirikiano kwa vita ambavyo havina uhalali wa kimataifa ni ukiukaji wa wazi wa hati ya Umoja wa Mataifa na wajibu wa Ujerumani kama taifa la amani.'
Naibu Kansela wa Ujerumani aliongeza kuwa Berlin haitaruhusu ardhi ya Ujerumani kutumika kwa vitendo vya upande mmoja na vya uvamizi. Msimamo huu umetolewa huku huduma ya utafiti ya Bunge la Ujerumani (Bundestag) pia katika tathmini yake ya hivi karibuni inaliona shambulio lolote dhidi ya Iran bila idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa halina uhalali wa kisheria.
Ulrich Thoden, mbunge wa upinzani katika Bunge la Ujerumani, ameitaka serikali ya Berlin izuie mara moja matumizi ya kituo cha Ramstein na akatahadharisha kwamba kuendelea mwenendo huu kutaifanya Ujerumani kushiriki katika uvunjaji wa sheria za kimataifa.
Mbali na mataifa hayo, Ufaransa pia imezuia ndege zinazobeba vifaa vya kijeshi kuelekea Israel kupita katika anga yake, na Italia kwa kuzingatia masharti ya kisheria, imefunga na kuizuia Marekani kufikia vituo vyake vya kijeshi.
Wachambuzi wa taasisi maarufu duniani pia wanayafuatilia mabadiliko haya kwa makini. Taasisi ya Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni (ECFR) imesema katika uchambuzi wake kwamba, msimamo huu ni mtihani wa hatima kwa Umoja wa Ulaya na imesisitiza kwamba, viongozi wa Ulaya lazima kwa pamoja na kwa uthabiti kabisa wajibu mashinikizo ya kiuchumi na kiusalama ya Washington ili kulinda uhuru wa umoja huo.
Kwa upande mwingine, jarida la Marekani la Politico likimnukuu Dr.Sanam Vakil, mtaalamu wa Mashariki ya Kati kutoka taasisi ya Chatham House, linaandika kwamba, hatua za kijeshi za Marekani zinaonyesha kupungua ushawishi na kuwekwa pembeni kwa nguvu za Ulaya katika eneo hilo. Hata hivyo, hali hii ya kusukumwa pembeni imeisogeza Ulaya kuelekea upande wa kujitegemea zaidi.
Mwishoni mwa mahojiano yake na Politico, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uhispania aliashiria kuongezeka ukosefu wa utulivu duniani na kutotabirika zaidi siasa za nje za Atlantiki, na kusisitiza kwamba, msimamo wa Uhispania sasa umegeuka kuwa 'mkondo mkuu ndani ya kambi ya Ulaya' na kwamba 'wakati wa uhuru na mamlaka ya kujitawala Ulaya sasa umewadia.
Hii hamu ya kujitegemea inazidi kuongezeka huku wachambuzi wa taasisi ya Elcano nchini Uhispania wakiona uamuzi wa Madrid kama hatari ya kimkakati inayoweza kuleta mashaka juu ya nafasi ya nchi hiyo ndani ya Shirika la NATO, lakini kwa wakati mmoja wanauona kama mfano kwa wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya wanaotaka kusimamisha vita vya upande mmoja.
Kwa ujumla, kile ambacho tumeshuhudia katika wiki za hivi karibuni si tofauti ndogo za kidiplomasia zilizotawanyika, bali ni mwanzo wa mpasuko wa kimkakati kati ya pande mbili za Atlantiki.
Uhispania na Ujerumani kwa kusimama dhidi ya tamaa na upendaji makuu wa kivita wa Marekani, zimeionyesha wazi Washington kwamba, haiwezi tena kutegemea msaada usio na masharti kutoka kwa washirika wake wa jadi. Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa, mabadiliko haya yana ujumbe ulio wazi nao ni kwamba, uvamizi wowote wa kijeshi utakuwa na gharama kubwa za kisiasa na vifaa, na jamii ya kimataifa — hata washirika wa karibu wa Marekani — hawana mwafaka wa pamoja kuhusu vita dhidi ya Iran.