Iran: Hakuna chombo kinachoweza kupita salama Hormuz bila idhini
-
Luteni Kanali Ebrahim Zolfaqari
Msemaji wa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ijulikanayo kama Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya amekanusha madai ya Marekani kwamba meli zinaendelea kupita kwa hali ya kawaida katika Lango Bahari la Hormuz, akisema hakuna chombo kinachoweza kuvuka kwa usalama njia hiyo ya kimkakati bila idhini na uangalizi wa Iran.
Luteni Kanali Ebrahim Zolfaqari alisema katika taarifa ya Alhamisi kwamba madai ya Marekani kuhusu kupita kwa kawaida kwa vyombo vya majini katika Lango-Bahari la Hormuz ni “ya uongo na yasiyo na msingi,” akiyataja kuwa ni ishara ya kukata tamaa na kushindwa kwa jeshi la Marekani.
“Lango-Bahari la Hormuz linasalia, kama ilivyokuwa zamani, chini ya usimamizi na udhibiti kamili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran,” amesema Zolfaqari, akiongeza kuwa hakuna meli ya kibiashara wala ya mafuta inayoweza kupita salama katika njia hiyo bila idhini na uangalizi wa vikosi vya kijeshi vya Iran.
Ameongeza kuwa Marekani na jeshi lake vimewahi kushuhudia mara kwa mara “nguvu na msimamo thabiti” wa wananchi wa Iran pamoja na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo.
Luteni Kanali Zolfaqari pia ameikosoa Marekani kwa kuendeleza chokochoko za kuyumbisha usalama katika eneo hilo.
Aliongeza kuwa vikosi vya ulinzi vya Iran vinafuatilia kwa karibu shughuli za Marekani na Israel katika eneo, na vitajibu tishio lolote “kwa nguvu na ukali zaidi kuliko hapo awali.”
Taarifa hiyo imesema vikosi vya ulinzi vya Iran vitaendelea kuchukua hatua za kulinda mamlaka ya kitaifa na maslahi ya nchi chini ya uongozi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei.
Marekani imekuwa ikiishambulia Iran tangu mapema Julai, baada ya Washington kukiuka masharti ya Hati ya Makubaliano ya Islamabad, ambayo ilikusudiwa kumaliza kabisa vita vilivyoanzishwa dhidi ya Iran na Marekani pamoja na utawala wa Israel mwishoni mwa Februari.
Makubaliano hayo yalitambua haki na mamlaka ya Iran juu ya Lango-Bahari la Hormuz. Hata hivyo, Marekani imekiuka mapatano hayo na kuanzisha mkondo usio salama karibu na pwani ya Oman.
Hatua hiyo ya Marekani, ambayo ni kinyume cha sheria, ilichochea jibu kali la Iran ambayo sasa inasimamia eneo hilo la kimkakati baharini. Iran imesisitiza kuwa harakati yoyote katika njia hiyo nyeti ya kimkakati lazima ifanywe kwa mujibu wa mipango na taratibu za Iran, kwa kuzingatia makubaliano hayo.