Siku ya Amani Duniani yagubikwa na vita vilivyoanzishwa na Marekani, Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141632-siku_ya_amani_duniani_yagubikwa_na_vita_vilivyoanzishwa_na_marekani_israel
Siku ya Amani Duniani, ambayo huadhimishwa kila Septemba 21, mwaka huu inakuja wakati ulimwengu ukikabiliwa na mfululizo wa vita na migogoro ya kiusalama inayozidi kuenea, huku Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ikiwa tena katika kitovu cha wasiwasi wa kimataifa.
(last modified 2026-09-22T09:38:16+00:00 )
Sep 22, 2026 03:28 UTC
  • Siku ya Amani Duniani yagubikwa na vita vilivyoanzishwa na Marekani, Israel

Siku ya Amani Duniani, ambayo huadhimishwa kila Septemba 21, mwaka huu inakuja wakati ulimwengu ukikabiliwa na mfululizo wa vita na migogoro ya kiusalama inayozidi kuenea, huku Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ikiwa tena katika kitovu cha wasiwasi wa kimataifa.

Septemba 21 huadhimishwa na Umoja wa Mataifa kama Siku ya Kimataifa ya Amani, siku iliyokusudiwa kusisitiza moja ya kanuni za msingi za jumuiya ya kimataifa: kuzuia vita, kukataa vitendo vya kikatili, na utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani.

Hata hivyo, maadhimisho ya mwaka huu yanakuja katika wakati ambapo pengo kati ya matamanio ya amani na uhalisia wa mambo linabaki kuwa kubwa na la kutisha. Migogoro ya kivita inaendelea katika maeneo kadhaa, huku eneo la Asia Magharibi likishuhudia ongezeko kubwa la mivutano kufuatia vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, sambamba na janga la kibinadamu lililosababishwa na utawala katili wa Israel huko Gaza.

Wazo la kutenga siku kwa ajili ya amani lilianzishwa kwa mara ya kwanza na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1981.

Tarehe 30 Novemba ya mwaka huo, Baraza Kuu lilipitisha Azimio namba 36/67, likianzisha Siku ya Kimataifa ya Amani. Maadhimisho ya kwanza yalifanyika Septemba 1982.

Uchokozi ulioanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28, 2026 umezua tena maswali ya msingi kuhusu uwezo wa taasisi za kimataifa kuzuia vita na kulinda raia.Gaza inawakilisha mtihani mwingine mkubwa kwa dhamira ya kimataifa ya amani. Utawala wa Israel ulianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo la Palestina Oktoba 2023 na hadi sasa utawala huo umeua Wapalestina wasipungua 73,000 wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Licha ya mipango ya kusitisha mapigano na juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kumaliza mgogoro, vitendo vya kikatili na mauaji ya raia yameendelea.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito kwa viongozi wa dunia na wananchi kuwekeza zaidi katika amani, akionya kuwa dunia kwa sasa inakabiliwa na ongezeko la migogoro, ghasia na mgawanyiko unaosababisha mateso makubwa kwa mamilioni ya watu. Katika ujumbe wake wa maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani 2026, Guterres pia amezitaka serikali na viongozi wa dunia kuimarisha diplomasia, mazungumzo, usuluhishi na operesheni za kulinda amani kama njia muhimu za kuzuia na kutatua migogoro.