Iran: Miinuko ya Golan ni sehemu isiyotenganishwa na ardhi ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140656-iran_miinuko_ya_golan_ni_sehemu_isiyotenganishwa_na_ardhi_ya_syria
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kwamba Miinuko ya Golan ni sehemu isiyotenganishwa na ardhi ya Syria, huku ikieleza kuunga mkono mapambano halali ya wananchi wa Palestina.
(last modified 2026-08-14T03:10:14+00:00 )
Aug 14, 2026 03:09 UTC
  • Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
    Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kwamba Miinuko ya Golan ni sehemu isiyotenganishwa na ardhi ya Syria, huku ikieleza kuunga mkono mapambano halali ya wananchi wa Palestina.

Tehran imesisitiza pia msimamo wake wa kuunga mkono haki za wananchi wa Palestina na mapambano yao ya kisheria kwa ajili ya kutetea haki zao.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema katika taarifa yale kwamba Miinuko ya Golan ni sehemu isiyotenganishwa na ardhi ya Syria.

Wizara hiyo pia imesema kwamba ardhi ya Palestina ni mali ya wananchi wa Palestina, na kwamba fikra za kibaguzi za utawala wa Kizayuni unaofanya mauaji ya kimbari haviwezi kubadilisha ukweli huo wa mambo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel kuhusu madai kwamba Miinuko ya Golan ya Syria ni mali ya Israel milele, pamoja na msimamo wake wa kupinga kuwepo taifa huru la Palestina.

Aidha katika taarifa yake, wizara hiyo imesema kuwa ardhi ya Palestina ni ya wananchi wa Palestina, na kwamba “mawazo ya kibaguzi” ya utawala wa Kizayuni hayawezi kubadilisha ukweli huo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza kuwa kiongozi wa “genge la kihalifu na la kimafia linalotawala katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu” hana nafasi ya kutoa maoni kuhusu kuanzishwa taifa huru la Palestina.

Sehemuu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, hatua ya hivi karibuni ya serikali ya Colombia ya kutambua mamlaka ya Israel kwa eneo la Golan linalokaliwa kwa mabavu haikubaliki na inalaaniwa vikali.

Wizara hiyo imesema hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, hususan kanuni ya kuheshimu mamlaka na umoja wa ardhi wa mataifa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hatua ya Colombia pia inapingana na kanuni inayotambulika katika sheria za kimataifa inayokataza kutambua matokeo yanayotokana na vitendo visivyo halali, na kwamba hatua hiyo inaweza kusababisha uwajibikaji wa kimataifa wa serikali ya Colombia.