Ecowas yataka kuwepo mkakati madhubuti wa kikanda wa kutokomeza malaria
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imetaka kuimarishwa mikakati ya kikanda ili kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria.
Jumuiya hiyo ilifanya Mkutano wake wa 27 wa Kawaida wa Mawaziri wa Afya huko Freetown, mji mkuu wa Sierra Leone, katika jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa malaria katika eneo la magharibi mwa Afrika.
Mkutano huo wa siku mbili wa ngazi ya juu wa nchi wanachama wa Ecowas umehuhudhuriwa pia na wawakilishi wa serikali, washirika wa kiufundi na kifedha, na wataalamu wa afya wa kikanda.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Julius Maada Bio wa Sierra Leone amesema kuwa mkutano huo unalenga kuimarisha hatua za pamoja dhidi ya mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za afya ya umma katika eneo la magharibi mwa Afrika.
Rais wa Sierra Leone amesisitiza kuwa ipo haja ya kuwa na mifumo imara, inayoendeshwa na data na ubunifu wa afya kuanzia stratejia za kudhibiti malaria hadi kuutokomeza kikamilifu ugonjwa huo.
Naye Austin Demby Waziri wa Afya wa Sierra Leone amesema kuwa hatua za kukabiliana na ugonjwa wa malaria duniani zimepungua tangu mwaka 2015, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua ufadhili na athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika kueneza ugonjwa huo.