Matokeo ya Kuendelea Vita: Marekani Iliyodhoofika na Iran Iliyoimarika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140680-matokeo_ya_kuendelea_vita_marekani_iliyodhoofika_na_iran_iliyoimarika
Seneta mmoja wa Marekani amekiri kuwa kuendelea vita kati ya Marekani na Iran kutapelekea Marekani kudhoofika na Iran kuimarika zaidi.
(last modified 2026-08-15T05:49:48+00:00 )
Aug 15, 2026 05:46 UTC
  • Matokeo ya Kuendelea Vita: Marekani Iliyodhoofika na Iran Iliyoimarika

Seneta mmoja wa Marekani amekiri kuwa kuendelea vita kati ya Marekani na Iran kutapelekea Marekani kudhoofika na Iran kuimarika zaidi.

Chris Murphy, Seneta wa chama cha Democratic, amekiri kuwa Rais Donald Trump wa Marekani ameshindwa katika vita na kwamba kuendelea kwa mgogoro huo wa kijeshi kutaiacha Marekani ikiwa dhaifu zaidi na Iran kuimarika zaidi. Katika mahojiano na NBC News siku ya Jumapili, seneta huyo kutoka jimbo la Connecticut amesema: "Ningeliunga mkono makubaliano ya kumaliza vita hivi na kufunguliwa tena Lango- Bahari la Hormuz. Niko tayari kuunga mkono makubaliano mabaya ili kumaliza vita hivi na kufunguliwa tena Lango hilo, kwa sababu makubaliano pekee yaliyopo kwa sasa ni ima mabaya au ya kutisha zaidi."

Murphy, mjumbe wa Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, ameongeza kuwa Trump anakabiliwa na machaguo yasiyofaa, hivyo lazima atafute njia ya kuleta utulivu katika masoko ya dunia na kupunguza gharama ya maisha kwa Wamarekani wa kawaida. Amesisitiza kuwa vita lazima vikome, kwani kila siku vinaiacha Marekani ikiwa dhaifu na Iran ikiwa na nguvu zaidi, huku watu wa hapa Marekani wakitatizwa na kupanda kwa bei ya bidhaa.

Kauli ya seneta huyu mashuhuri wa chama cha Democrats nchini Marekani haiwakilishi tu msimamo wa kisiasa wa chama, bali ni tathmini ya kimkakati ya mgogoro ambao umedumu kwa karibu miezi sita sasa. Ili kuelewa kina cha uchambuzi huu, ni lazima tuchunguze sababu za kudhoofika nafasi ya Marekani na wakati huo huo kuimarika Iran, katika mgogoro huu kupitia mitazamo mitatu: Mchoko wa kijeshi, gharama za kiuchumi na mkwamo wa kimkakati.

Sababu tatu kuu za kudhoofika Marekani katika vita dhidi ya Iran zinaweza kubainishwa kama ifuatavyo: 1. Kudhoofika kwa nguvu za kijeshi kutokana na kupungua kwa akiba ya silaha na kuongezeka hatari ya kimkakati: Vita vya kisasa vinavyojumuisha makabiliano makali vinahitajia matumizi makubwa ya silaha zenye usahihi wa hali ya juu. Katika mahojiano hayo, Murphy amefichua kuwa Marekani imetumia karibu asilimia 80 ya makombora yake ya kuzuia mashambulizi ya anga na sehemu kubwa ya makombora yake ya aina ya Tomahawk. Hii inaashiria kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani na washirika wake inakabiliwa na uhaba mkubwa wa silaha hizo. Kwa mujibu wa Murphy, shinikizo hili kubwa la kijeshi "limezipa Russia na China ujasiri wa kufikiria hatua ambazo huko hazingefikirika, kwa sababu tu tumekosa uwezo wa kujilinda sisi wenyewe na washirika wetu." Kwa maneno mengine, vita ambavyo awali vilikusudiwa kuidhibiti Iran sasa vimepunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Marekani wa kukabiliana na vitisho vingine vya kimataifa.

2. Gharama za Kiuchumi: Kuanzia uwanja wa vita hadi meza za chakula za Wamarekani, taathira za kiuchumi za vita hivi zinavuka mipaka ya bajeti ya Pentagon na kuathiri moja kwa moja maisha ya kila siku ya raia wa Marekani. Murphy anasisitiza kuwa kila siku ya vita inayopita, familia za Marekani hukabiliwa na bei ya juu ya bidhaa za msingi. Kufungwa kwa Lango-Bahari la Hormuz, ambapo karibu sehemu ya tano ya mafuta ya dunia hupitia, kumesababisha moja kwa moja kupanda kwa bei ya nishati na kuchochea mfumuko wa bei kote nchini Marekani. Tafiti zinaonyesha kuwa takriban asilimia 70 ya Wamarekani wanataka vita hivi visimamishwe mara moja, na kwamba familia nyingi ziko ukingoni mwa kufilisika kifedha.

3. Mkwamo wa kimkakati na kunasa katika hali ngumu isiyo na njia ya kukimbilia: Baada ya miezi sita ya mapigano na Iran, hali imefikia mkwamo kamili. Jenerali Dan Keane, afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la Marekani, ametoa onyo la siri kwa Ikulu ya Marekani kwamba ni lazima upatikane "mkakati wa kujiondoa," akitambua kuwa kuongeza hatua za kijeshi si tu kwamba hakutaleta matokeo chanya, bali pia hakutafanikisha malengo yaliyowekwa kwa kutumia mashambulizi ya anga pekee. Katika kipindi hiki, Marekani imetumia mbinu mbalimbali, ikiwemo takriban siku 40 za mashambulizi makali ya mabomu, mzingiro wa majini wa miezi miwili, kusainiwa makubaliano ya usitishaji vita na siku 13 za mashambulizi makali ya ziada, lakini hakuna hata hatua moja kati ya hizo iliyofanikiwa kuilazimisha Tehran isalimu amri. Daniel Davis, kanali mstaafu wa jeshi, ameandika katika uchambuzi wake kwamba "Marekani imeshindwa katika vita dhidi ya Iran katika ngazi ya kimkakati, na hakuna hatua tutakayochukua kuanzia sasa na kuendelea inayoweza kubadili matokeo haya."

Hii ni katika hali ambayo Iran imefanikiwa kuimarisha nguzo tatu za nguvu zake katika mzozo huu:

1. Ushawishi wa kijiopolitiki kupitia udhibiti wa Lango-Bahari la Hormuz. Silaha yenye nguvu kubwa zaidi ya Iran katika mapambano haya sio makombora yake, bali ni eneo lake la kijiografia. Ili kukabiliana na ubabe wa Marekani angani na baharini, Iran imetumia vizuri zana yake kuu ya kimkakati isiyo ya kawaida ambayo ni udhibiti wa Lango-Bahari la Hormuz. Tehran imeweka wazi kuwa lango hilo halitafunguliwa tena hadi pale masharti yake yatakapotekelezwa. Masharti haya ni pamoja na kuondolewa vikwazo, kukomeshwa uhasama, kuondolewa mzingiro dhidi ya bandari za Iran, malipo ya fidia ya vita, na kuachiliwa bila masharti mali za Iran zinazozuiliwa na nchi za kigeni, hasa hasa Marekani.

2. Ustahimilivu wa kijeshi kupitia matumizi ya "miji ya makombora" ya chini ya ardhi na uwezo wa vita vya kuchosha: Mkakati wa kijeshi wa Iran umejengeka kwenye msingi kwamba Marekani haiwezi kuharibu kabisa miundombinu yake ya kijeshi na nyuklia kupitia mashambulizi ya anga pekee. Kwa kipindi cha miongo miwili, Iran imejenga mtandao mkubwa wa vituo vya chini ya ardhi, vinavyojulikana kama "miji ya makombora", ambavyo hutumika kama maeneo ya kuhifadhi, kurusha, na hata uzalishaji endelevu wa ndege zisizo na rubani za masafa marefu na makombora ya balistiki. Kwa maoni ya Davis, "hakuna kampeni ya kawaida ya mashambulizi ya mabomu, hata iwe kali au ndefu kiasi gani, ambayo inaweza kuharibu vituo vyote vya chini ya ardhi vya Iran." Uwezo huu wa kimkakati unaipa Iran fursa ya kupandisha kiwango cha mgogoro hadi kufikia hatua ambayo itaitwisha Marekani gharama kubwa, bila kuathiri uwezo wake yenyewe wa kulipiza kisasi.

3. Kupanda kwa hadhi ya kijiopolitiki kutoka kuwa mchezaji na mdau wa kikanda tu hadi kuwa mhusika wa ngazi ya kimataifa. Kuendelea kwa mzozo huu hakujadumisha tu nguvu ya ndani ya Iran bali pia kumeleta mabadiliko makubwa katika ngazi ya kikanda. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa mkakati wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi au ukitaka Mashariki ya Kati, umefeli na kwamba vita hivi vimegeuka kuwa "janga kubwa la kimkakati" kwa nchi hiyo ya Magharibi. Badala ya kudhoofika, Iran imejiimarisha zaidi katika nyanja mbalimbali za kiintelijensia na ushawishi wa kikanda, na hivyo kuboresha zaidi hadhi yake.

Hatua nyingine muhimu zaidi ni kuundwa haraka muungano wa ulinzi wa pande tatu za Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan, hatua ambayo baadhi ya wachunguzi wanaiona kama ishara ya Marekani "kukimbia" kutoka Asia Magharibi.

Karibuni tu, Marekani imekuwa na uwepo katika eneo hili kupitia mtandao mpana wa kambi za kijeshi, lakini leo, washindani na vilevile washirika wake wa zamani wanatathmini na kuhoji udharura wa uwepo huo wa Marekani katika eneo.

Hatimaye, kauli ya Seneta Murphy ni muhimu kwa sababu inaelezea uhalisia ambao wanasiasa wengi wa Marekani hawataki kuukubali, nao ni kwamba, ubora wa kijeshi inaodaiwa kuwa nao Marekani katika mzozo na Iran haujageuka kuwa ushindi wa kimkakati kwa nchi hiyo. Vita hivi si tu vimeshindwa kufikia malengo yaliyotangazwa na Trump, bali vimekuwa kichocheo cha kushuka hadhi ya Marekani duniani na wakati huohuo, kuimarisha zaidi hadhi ya Iran kieneo na kimataifa.