Araghchi: Bado Hatujachukua uamuzi wowote wa kuanzisha upya mazungumzo na Marekani
-
Araghchi: Bado Hatujachukua uamuzi wowote wa kuanzisha upya mazungumzo na Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, Tehran bado haijachukua uamuzi wowote wa kuanza tena mazungumzo na upande wa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, akizungumzia hali ya sasa ya Mkataba wa Makubaliano ya Kusitisha Vita wa Islamabad, amesema:
“Katika hati ya makubaliano ya Islamabad, ‘kumalizika kwa vita’ kulitangazwa, na hakuna kusitishwa mapigano ambako kunapaswa kuongezwa muda. Kilichowekwa ni kipindi cha siku 60 cha kufanya mazungumzo kwa ajili ya kufikia makubaliano ya mwisho. Hata hivyo, Marekani ilikiuka makubaliano hayo na mapigano yakaanza tena.”
Abbas Araghchi ameongeza kuwa, Qatar na Pakistan, kama wapatanishi, wanabadilishana tu ujumbe na kuwasiliana, lakini hilo halimaanishi kwamba kuna mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na Iran. Alisisitiza kuwa Iran bado haijafanya uamuzi wa kuanza tena mazungumzo na utawala wa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifafanua kuwa, mazungumzo ya Iran na Oman ni suala tofauti kabisa, linalohusu masuala ya kiufundi ya kuainisha njia za baharini katika Mlango wa Hormuz na namna meli zitakavyopita.
Alisema njia zilizokuwa zikitumika hapo awali hazifai tena, hivyo kwa sasa wanaandaa njia ya muda ambayo baadaye itabadilishwa kuwa njia ya kudumu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisisitiza kuwa mazungumzo ya kiufundi na Oman na suala la kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz ni mambo mawili tofauti. Alisema hata baada ya njia hiyo kuainishwa, kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz kutategemea kutimizwa masharti mengine ambayo Marekani inapaswa kuyaheshimu na kuyatekeleza.