Iran yaitaka Ufaransa kutoa maelezo kuhusu mienendo “haramu” ya wanadiplomasia wake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140686-iran_yaitaka_ufaransa_kutoa_maelezo_kuhusu_mienendo_haramu_ya_wanadiplomasia_wake
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imeionya Ufaransa dhidi ya kuingilia mambo ya ndani ya taifa hili, ikisema kuwa Paris inapaswa kutoa maelezo kuhusu mienendo na shughuli haramu za wanadiplomasia wake.
(last modified 2026-08-15T11:02:53+00:00 )
Aug 15, 2026 10:57 UTC
  • Iran yaitaka Ufaransa kutoa maelezo kuhusu mienendo “haramu” ya wanadiplomasia wake
    Iran yaitaka Ufaransa kutoa maelezo kuhusu mienendo “haramu” ya wanadiplomasia wake

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imeionya Ufaransa dhidi ya kuingilia mambo ya ndani ya taifa hili, ikisema kuwa Paris inapaswa kutoa maelezo kuhusu mienendo na shughuli haramu za wanadiplomasia wake.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumamosi, wizara hiyo imesema vikosi vyake vilibaini kuwepo wanadiplomasia wawili wa Ufaransa katika eneo la siri la kufanyia mikutano, wakati vikosi hivyo vilipokuwa vinatekeleza amri ya mahakama ya kuwakamata washukiwa wawili katika kesi kubwa inayohusisha kupenyeza kwa wageni na kuingilia mambo ya ndani ya nchi.

Mnamo Julai 2026, wanadiplomasia wawili wa Ufaransa walizuiliwa kwa muda mfupi mjini Tehran baada ya kubainika kuwa walikuwa katika mkutano uliohusishwa na uchunguzi wa kiusalama.

Ufaransa ilivishutumu vikosi vya usalama vya Iran kwa kuwatendea vibaya wanadiplomasia hao, huku Tehran ikipinga madai hayo na kusema kuwa walihojiwa kutokana na “mienendo isiyo ya kawaida.”

Wizara hiyo ilisema wanadiplomasia hao wawili walikuwa na “historia ndefu ya ukiukaji wa sheria na mienendo inayokwenda kinyume na sheria za ndani pamoja na wajibu wao wa kidiplomasia.”

Baada ya kuthibitisha utambulisho wao, suala hilo liliwasilishwa kwa Wizara ya Mambo ya Nje, na wanadiplomasia hao walikabidhiwa kwa balozi wa Iran nchini Ufaransa, mbele ya maafisa wa polisi wanaoshughulikia masuala ya kidiplomasia, ilisema taarifa hiyo.

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran hiyo pia iligusia sheria iliyopitishwa na Ufaransa mwaka 2024 kwa lengo la kuzuia uingiliaji wa kigeni, ikisema kwamba hivyo basi Paris inafahamu vyema kanuni zinazotumika katika kupiga marufuku uingiliaji wa mataifa ya kigeni.

Taarifa hiyo iliitaka serikali ya Ufaransa ijikite katika kutatua matatizo ya ndani ya nchi hiyo na kushughulikia mahitaji ya kijamii ya wananchi wake, badala ya kuingilia mambo ya nchi huru.