Umoja wa Mataifa: Wakimbizi 650,000 Sudan Kusini hatarini kukosa chakula
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140682-umoja_wa_mataifa_wakimbizi_650_000_sudan_kusini_hatarini_kukosa_chakula
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa zaidi ya wakimbizi 650,000 Sudan Kusini wako hatarini kukosa chakula katka wiki chache zijazo.
(last modified 2026-08-15T10:56:10+00:00 )
Aug 15, 2026 10:54 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Wakimbizi 650,000 Sudan Kusini hatarini kukosa chakula
    Umoja wa Mataifa: Wakimbizi 650,000 Sudan Kusini hatarini kukosa chakula

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa zaidi ya wakimbizi 650,000 Sudan Kusini wako hatarini kukosa chakula katka wiki chache zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa hatari hiyo inatokana na ukosefu mkubwa wa fedha unaoweza kuwalazimisha kurejea Sudan, eneo lenye mzozo.

Mesfin Degefu msaidizi wa Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa Sudan Kusini amesema kuwa, iwapo ufadhili wa haraka hautapatikana, hakuna mkimbizi atakayepata msaada wa chakula kuanzia mwezi Oktobam waka huu.

Ripoti zinasema kuwa, Sudan Kusini inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula ambapo zaidi ya watu milioni 7.8 nchini humo wameathiriwa na njaa wakati watoto milioni 2.2 wakikabiliwa na utapiamlo uliopindukia.

Licha ya changamoto hizo, nchi hiyo inapokea karibu wakimbizi 3,000 kila wiki kutoka nchi jirani ya Sudan inayokabiliwa na vita. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa, mgao wa mwisho wa chakula kwa wakimbizi 240,000 walio hatarini zaidi nchini Sudan Kusini utafanyika mwezi Septemba endapo hakutapatikana ufadhili mpya wa dharura baada ya hapo.

Sudan Kusini ilipata uhuru kutoka Sudan tarehe 9 Julai 2011, baada ya wananchi kupiga kura kwa wingi kuunga mkono kujitenga. Hata hivyo, uhuru haukuondoa migawanyiko ya kisiasa na kikabila iliyokuwepo nchini.

Mgogoro mkubwa ulianza Desemba 2013, baada ya mzozo wa madaraka kati ya Rais Salva Kiir Mayardit na aliyekuwa Makamu wa Rais Riek Machar. Kiir alimshtumu Machar kwa kupanga mapinduzi, jambo ambalo Machar alilikana. Mapigano yaliyoanza Juba yalienea katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Ingawa chanzo cha mgogoro kilikuwa kwa kiasi kikubwa mivutano ya kisiasa na kugombea madaraka, mapigano yalichukua sura ya kikabila. Salva Kiir anatoka jamii ya Dinka huku Riek Machar akiwa anatoka jamii ya Nuer.