Namna Ulaya Ilivyochoshwa na Uchukuaji Hatua wa Upande Mmoja wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i137974-namna_ulaya_ilivyochoshwa_na_uchukuaji_hatua_wa_upande_mmoja_wa_marekani
Kuendelea kupanuka ufa wa mpasuko uliojitokeza kati ya Ulaya na Marekani kumezifanya serikali za Ulaya zichoshwe na mienendo ya udhalilishaji ya Trump na uchukuaji wake wa hatua wa upande mmoja.
(last modified 2026-04-26T09:26:44+00:00 )
Apr 26, 2026 09:10 UTC
  • Namna Ulaya Ilivyochoshwa na Uchukuaji Hatua wa Upande Mmoja wa Marekani

Kuendelea kupanuka ufa wa mpasuko uliojitokeza kati ya Ulaya na Marekani kumezifanya serikali za Ulaya zichoshwe na mienendo ya udhalilishaji ya Trump na uchukuaji wake wa hatua wa upande mmoja.

Alipohojiwa na televisheni ya Aljazeera na kuulizwa kama muungano wa kijeshi wa NATO unayachukuliaje matamshi ya waziri wa vita wa Marekani aliyesema, kwa miongo kadhaa Ulaya na Asia zimekuwa zikinufaika na msaada wa Marekani na kwamba zama za kutumia msaada huo bila malipo zimemalizika, afisa wa zamani wa NATO Nicholas Williams amesema: "Mimi ninaamini kwamba watu wa Ulaya na Wacanada wamechoshwa na matusi haya; na kwa kweli maneno haya yanaudhi."
Afisa huyo wa zamani wa NATO ameongeza kuwa: "Marekani ilianzisha vita dhidi ya Iran bila kushauriana na Ulaya, Canada au NATO. Akthari ya nchi hizi zinavichukulia vita hivyo kuwa havina uhalali wa kisheria." Serikali za Ulaya katika ngazi mbalimbali na kwa lugha tofauti zimesema, Marekani haifanyi mambo kwa kufuata uratibu unaotawala mfumo wa sheria zinazosimamia ushirikiano wa kiusalama wa nchi wanachama wa NATO huku ikitarajia washirika wake katika shirika hilo waiunge mkono pale inapokumbana na mkwamo. Kutokana na uhusiano walionao na Trump, wanachama wote wa NATO, wamepinga ombi la kuungana na Marekani katika vita dhidi ya Iran.
Baadhi ya serikali za Ulaya zimetamka kinagaubaga kuwa ‘hivi si vita vyetu’ na kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni zimeanzisha vita hivyo bila ya kuwa na mpango wowote maalumu unaoendana na uhalisia. Lawama za serikali za Ulaya kwa Trump zimeibua wasiwasi katika baadhi ya duru za utawala ndani ya Marekani. Kwa sababu kuongezeka ufa wa mpasuko kati ya washirika wa pande mbili za Atlantiki hatimaye kutaharakisha mporomoko na kutoweka kwa zama za kutawala sauti moja tu ya Marekani. Kurt Volker, balozi wa zamani wa Marekani katika shirika la kijeshi la NATO ameashiria tofauti zilizozuka hivi karibuni kati ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na kueleza kwamba, kukosolewa hadharani sera za serikali ya Washington kuhusiana na vita dhidi ya Iran kunaweza kuwa na matokeo hasi kwa uhusiano wa pande mbili za Atlantiki.
Pamoja na hayo, Volker anasema, hata kama baadhi ya serikali za Ulaya zinachukulia hatua za Washington kuwa ni za "makosa" au "zenye matokeo ya kutia wasiwasi" lakini ingekuwa bora kama mitazamo hiyo isingebainishwa hadharani. Mwanadiplomasia huyo wa zamani wa Marekani anasema, ukosoaji wa hadharani unaweza kufuatiwa na mjibizo mkali wa Rais Trump na kupanua wigo wa nongwa na malalamiko ya Washington katika nyuga zingine za ushirikiano. 

Hata hivyo kinyume na anavyodhani Volker, mpasuko uliopo kati ya Marekani na washirika wake ni mkubwa mno kuweza kudhibitiwa kwa kujichunga na utoaji kauli za kumkasirisha Trump.
Wataalamu na wanamikakati wengi wa Ulaya na Marekani wanakiri kuwa, kama hatutasema kwamba NATO imeshakufa, basi inaelekea kidogo kidogo kwenye hatua ya kukata roho. Juhudi zinazofanywa na serikali za Ulaya za kufikia hatua ya kuwa na mfumo wa kujitegemea wa usalama zinapaswa kutathminiwa kwa kuzingatia hali hii tete inayoshuhudiwa katika mkataba wa NATO. Katika ziara yake nchini Ugiriki, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesisitizia haja ya kuibadilisha Ulaya kuwa chombo chenye nguvu halisi duniani na kuongeza nafasi yake katika kutatua migogoro ya kimataifa. Akiashiria kubadilika kwa muelekeo wa Marekani, Rais wa Ufaransa ametangaza kwamba sera ya "Marekani Kwanza" imekuwa ikifuatiliwa mtawalia katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, na kuonyesha kwamba Ulaya si kipaumbele tena cha kimkakati kwa Washington.
Macron amesisitiza kuwa muelekeo huo hauhusiani na serikali fulani tu, bali ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa Marekani unaozingatia kwanza maslahi ya ndani na kisha ushindani baina yake na China. Rais wa Ufaransa ameendelea kubainisha kuwa, kwa kutambua ukweli huo, inapasa Ulaya ichukue hatua za kuimarisha uhuru na kujitegemea kwake kimkakati na kuimarisha nafasi yake katika mfumo wa kimataifa kwa kuongeza kasi na wigo wa uchukuaji maamuzi. Mtazamo huu ni tofauti na ule wa Waziri Mkuu wa Italia Giulia Meloni. Yeye amesisitizia haja ya kudumishwa mshikamano wa NATO na kutoa wito wa Ulaya kuwa na nafasi na mchango mkubwa katika muungano huo. Jarida la Wall Street Journal, limefanya uchanganuzi wa mpasuko uliopo kati ya Ulaya na Marekani na kuandika: Ulaya inaandaa kimya kimya mpango wa kutoa msukumo kwa NATO iwapo Trump ataiondoa Marekani katika shirika hilo au kupunguza uungaji mkono wake.
Fikra hiyo inalenga kuufanya muungano huo wa kijeshi uongozwe zaidi na Ulaya, kwa kufika hadi ya wakati mwingine kuitwa "NATO ya Ulaya," ili bara hilo liendelee kuwa na uwezo wa kujilinda na kujihami. Hata hivyo, Ulaya hii iliyopo haionyeshi kwamba inaweza kuwa kitu kimoja na kufikia kwenye muunganiko wa kiusalama wa kiwango hata kinacholingana na NATO.../