Kwa Nini Chuki Dhidi ya Israel Zinaendelea Kuongezeka Ndani ya Marekani?
Chama cha Democrat nchini Marekani hivi sasa kinazihama enzi za uungaji mkono wake wa jadi kwa utawala bandia wa Israel na kuhamia kwenye zama za kupingana vikali na utawala huo.
Gazeti la Wall Street Journal linalochapishwa nchini humo limeandika katika ripoti yake kwamba: katika kipindi cha miaka miwili, idadi ya maseneta wa Marekani wanaounga mkono vikwazo vya silaha dhidi ya baraza la mawaziri lenye msimamo mkali la waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu imeongezeka maradufu. Kwa sasa, utawala wa Kizayuni ndio mtihani mpya kwa chama cha Democrat nchini Marekani, na Seneta Bernie Sanders anaongoza vuguvugu la mabadiliko ya msimamo ulio dhidi ya baraza la mawaziri la Netanyahu.
Mnamo mwaka 2024, maseneta 19 wa chama cha Democrat walimuunga mkono Sanders katika kura ya kupinga kumpatia msaada wa kijeshi wakati wa vita mshirika huyo wa Marekani. 2025, maseneta 24 walifanya vivyo hivyo. Na katika upigaji kura wa mwaka huu, huku Marekani na utawala wa Kizayuni zikiwa zimeshirikiana pamoja kuanzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran, maseneta 40 kati ya 47 wa chama cha Democrat waliungana na Sanders kupiga kura dhidi ya Israel.
Wall Street Journal limeandika, kwa kawaida, utawala wa kizayuni unaungwa mkono na vyama vyote viwili vikuu vya siasa nchini humo vya Democrat na Republican, na wakosoaji wa sera za utawala huo wanapatikana ndani ya vyama vyote viwili, lakini kinachoshuhudiwa hivi sasa ndani ya mrengo wa kushoto yaani chama cha Democrat hakiwezi kukanushika, nacho ni kwamba; kumuunga mkono mshirika wa karibu zaidi wa Marekani katika Mashariki ya Kati kwa sasa kunahatarisha mustakabali wa kila mtu ndani ya chama hicho.
Kuna mtazamo ndani ya jamii ya Marekani kwamba Trump amenasa kwenye mtego wa vita nchini Iran kutokana na kufuata sera za kushupalia vita za Netanyahu. Netanyahu na Trump walikuwa wakidhani kwamba wataweza ndani ya muda wa siku nne tu kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Lakini kinyume na dhana hiyo, Iran iliibuka na ushindi katika kukabiliana na moto wa vita uliowashwa na utawala wa Kizayuni na Marekani. Kambi na vituo vyote vya kiintelijensia, kijasusi na kiusalama vya Marekani katika eneo na vya utawala wa kizayuni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel viliandamwa na msururu wa mashambulio na vipigo vikali vya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran. Vipigo hivyo vilimkoroga na kumkanganya pia Trump, kiasi cha kusikika saa moja anazungumzia kuangamizwa vikosi vya wanamaji, vya anga na vya nchi kavu vya Iran pamoja na vituo vyake vya makombora, kisha saa nyengine akaibuka na pendekezo la kufanya mazungumzo ili kufikia makubaliano na Tehran.

Kinachodhihirika kutokana na kauli hizo zinazogongana za upayukaji na uropokaji ni kukwama na kukata tamaa Trump kuhusiana na mapambano ya hamasa ya siku 40 ya Wairani ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni na Marekani.
Kupitia usitishaji vita na miito ya mazungumzo, Trump anataka kukitia mkononi kupitia meza ya mazungumzo kile ambacho hakuweza kukipata kwa njia ya vita. Rais huyo mwenye majivuno na majigambo wa Marekani anataka kuufanya uchokozi wa kijeshi alioanzisha dhidi ya Iran uonekane kuwa ni mafanikio na kulitumia hilo kama turufu ya kupatia umaarufu mbele fikra za umma ndani ya Marekani. Lakini ukweli ni kwamba, Trump amefikia kwenye mkwamo katika pande zote mbili za kijeshi na kidiplomasia.
Matokeo ya mkwamo huo ni kupanda kwa bei ya petroli, kuongezeka ughali wa maisha, kufifia umaarufu wa Trump ndani ya Marekani, na kuongezeka chuki dhidi ya Israel. Bila shaka kabla ya hapo, chuki dhidi ya utawala bandia wa Israel zilikuwa tayari zimeshaongezeka sana baada ya utawala huo kuuvamia Ukanda wa Ghaza na kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, kiasi kwamba vyombo vya usalama vya Marekani havikuweza hata kwa kutumia kisingizio cha kukabiliana na chuki dhidi ya Mayahudi, kulizima moja kwa moja wimbi kubwa lililoibuka ndani ya nchi hiyo la waungaji mkono wa wananchi madhulumu wa Palestina na wanaouchukia vikali utawala wa kizayuni wa Israel. Kwa sababu hiyo, serikali ya Marekani ikaishia kuwaandama na kuwafukuza wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu wanaowaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.
Hivi sasa, na baada ya kushirikiana na utawala wa kizayuni kuanzisha vita vya siku 40 dhidi ya Iran, utawala wa Trump umeibebesha Marekani mzigo wa gharama kubwa; yenye uzito zaidi ikiwa ni kuporomoka haiba na heshima ya Marekani na kuagana na zama za kuwepo kijeshi katika Ghuba ya Uajemi. Cheche za pigo hilo kubwa zimewasha moto mkali wa ukosoaji dhidi ya Trump na kulifanya suala la kutengana na Israel kuwa na kipaumbele maalumu cha kisiasa na kiusalama ndani ya duru za ngazi za juu za utawala Marekani.../