Ni ipi nafasi ya pande za kigeni katika mgogoro wa Sudan?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133130-ni_ipi_nafasi_ya_pande_za_kigeni_katika_mgogoro_wa_sudan
Vita nchini Sudan vimechukua sura mpya kufuatia kuendelea uingiliaji kati wa nchi ajinabi nchini humo na kudhibitiwa mji wa Al Fasher na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 13, 2025 09:25 UTC
  • Ni ipi nafasi ya pande za kigeni katika mgogoro wa Sudan?

Vita nchini Sudan vimechukua sura mpya kufuatia kuendelea uingiliaji kati wa nchi ajinabi nchini humo na kudhibitiwa mji wa Al Fasher na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Mamia ya watu wameuawa na ripoti zinaarifu kunyongwa watu na kujiri mauaji ya halaiki katika maeneo yanayodhibitiwa na wanamgambo wa RSF ya mji wa Al Fasher. Hii ni katika hali ambayo Minni Arko Minnawi, Gavana wa Darfur na kiongozi wa Harakati ya Ukombozi wa Sudan ametuma ujumbe katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Zaidi ya asilimia 85 ya wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ni mamluki kutoka nje. Huenda watu wengi hawajue ukweli huu lakini unadhihirisha kwamba kundi hilo si la kizalendo na tishio kubwa kwa mustakabali na umoja  wa ardhi ya Sudan." Minnawi ameeleza kuwa wanapasa kukabiliana na uingiliaji wa pande na nchi ajinabi katika vita vya ndani vinavyojiri Sudan na kusisitiza kuwa umoja wa kitaifa unapasa kuimarishwa katika jeshi la Sudan ili kulinda mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo. 

Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa, zaidi ya watu 150,000 wamepoteza maisha katika mapigano nchini Sudan na takriban watu milioni 12 wameyakimbia makazi yao katika kile kilichotajwa na Umoja wa Mataifa kuwa maafa makubwa zaidi ya binadamu duniani.

Baada ya kutekwa mji wa Al Fasher na kikosi cha RSF, mustakbali wa Sudan ambayo wakati fulani ilikuwa ikijulikana kama nchi kubwa zaidi na kapu la chakula la Ulimwengu wa Kiarabu, upo hatarini huku weledi wengi wa mambo wakitahadharisha kuhusu hatari ya kujitenga maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo.  Kuanguka Al Fasher, mji ambao ulikuwa kituo kikuu cha mwisho cha kanda nje ya udhibiti wa RSF, ni mabadiliko ya jiografia ya kisiasa na tukio kubwa; na wakati huo huo ni  mwanzo wa awamu mpya ambayo, ikiwa itaendelea, itasababisha kugawanyika nchi nzima ya Sudan. Kuangukia mji wa Al Fasher mikononi mwa wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kunatoa fursa kwa waasi hao kufikia kivuko muhimu kilichoko katika mpaka kati ya Chad na Libya; huku suala la uingiliaji wa nchi ajinabi huko Sudan ikiwa kadhia nyeti. 

Wanamgambo wa RSF 

Kwa hakika, hali tete ya ndani ya nchi hiyo na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha RSF yameibua mazingira ambayo madola ya kieneo na kimataifa yanafanya kila yawezalo ili kuathiri matukio ya kisiasa na kijeshi nchini Sudan.

Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ambacho awali kiliasisiwa kwa lengo la kukabiliana na machafuko na waasi wa ndani huko Sudan, hivi sasa kimekuwa moja ya wachezaji wakuu wa kijeshi nchini humo. Aghalabu ya wanamgambo wa kundi hilo wametumwa Sudan wakitokea katika nchi jirani kama Chad na Eritrea. Ukweli huu unaonyesha kuwa mgogoro wa Sudan si suala la ndani tu, bali mgogoro huo umekuwa uwanja wa ushindani kati ya wachezaji wa nje wanaowania kupata ushawishi na udhibiti huko Sudan na katika ukanda wa Kaskazini mwa Afrika.

Uingiliaji wa nchi mbalimbai ajinabi katika mgogoro wa Sudan zikiwemo nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia na nchi za Magharibi kama Marekani na Umoja wa Ulaya, pia unaonekana waziwazi. Nchi hizi zimeingia kwenye mgogoro wa Sudan kwa malengo tofauti. Kwa mfano, Imarati ambayo huko nyuma ilizidisha ushawishi wake wa kiuchumi na kisiasa nchini Sudan kwa kuwekeza katika migodi ya dhahabu na katika rasilimali nyinginezo, inajulikana kuwa miongoni mwa wachezaji wakuu tangu kuanza kwa vita huko Sudan. Imarati imekuwa ikiwapatia wanangambo wa RSF   aina mbalimbali za silaha, msaada fedha na suhula za kilojistiki. 

Saudi Arabia pia inataka kuimarisha nafasi yake nchini Sudan, kwa sababu inaihesabu nchi hiyo kuwa mshirika wake wa kimkakati mbele ya vitisho vya pamoja; kwa msingi huo, kwa upande mmoja, inaliunga mkono Jeshi la Sudan, na kwa upande mwingine, inajaribu kuzuia kusambaa hali mchafukoge huko Sudan na athari zake hasi kwa usalama wa kikanda. 

Mbali na uingiliaji kati wa kikanda, madola makubwa duniani pia yanahusika katika mgogoro wa Sudan. Uingiliaji wa Marekani na Umoja wa Ulaya katika mgogoro wa Sudan zaidi unafanywa kwa sababu za kisiasa na kimkakati. Nchi hizi hasa baada ya kupinduliwa Omar al-Bashir mwaka 2019, zinadai kuwa zinaunga mkono suala la kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia nchini Sudan na kurejesha demokrasia na utawala wa sheria. Wakati huo huo Washington na Brussels zimesema kuwa zina wasiwasi kuhusu machafuko yanayoendela nchini Sudan na kuingia katika nchi jirani na vitisho vya  makundi ya kigaidi katika eneo hilo. Hata hivyo, uingiliaji wa nchi ajinabi umezidisha mgogoro wa ndani na kusababisha migawanyiko zaidi nchini Sudan. 

Omar Hassan al Bashir 

Vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan sasa vimekuwa nyeti kwa mustakabali wa nchi hiyo na kanda nzima kwa ujumla. Wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) ambao wanaungwa mkono pakubwa kutoka nje, ni tishio kubwa kwa umoja wa Sudan. Kundi hilo linafanya kila liwezalo ili si tu kuimarishe zaidi ushawishi wake, bali pia yumkini likaandaa mazingira ya kusambaratika Sudan; nchi yenye tajiri na nafasi ya kijiopolitiki. Dalia Abdulmunim, mchambuzi wa siasa za Sudan anasema: Hii ni vita ya maamuzi. Kikosi cha RSF kinaweza kujitangazia uhuru au kushinikiza kuganywa Sudan.

Katika hali kama hii, inaonekana kuwa upo udharura wa kukomeshwa kikamilifu uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya Sudan, na kuwaacha Wasudani wenyewe watafute njia za kutatua mgogoro unaoisibu nchi yao ili kurejea katika amani ya kudumu.