Rais wa Burkina Faso atoa tamko kuhusu mivutano ya madaraka nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140108-rais_wa_burkina_faso_atoa_tamko_kuhusu_mivutano_ya_madaraka_nchini_humo
Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore, ametoa kauli nzito inayolenga kukomesha uvumi wa kuwepo kwa mivutano ya madaraka ndani ya safu za uongozi wake, akisisitiza dhamira yake ya kusalia kama kiongozi mkuu pekee wa taifa hilo. Traore aliwaambia viongozi wa jamii hivi karibuni mjini Ouahigouya, kaskazini mwa nchi hiyo kwamba: “Meli haiwezi kuwa na manahodha wawili,”
(last modified 2026-07-23T11:49:10+00:00 )
Jul 23, 2026 11:47 UTC
  • Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore
    Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore

Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore, ametoa kauli nzito inayolenga kukomesha uvumi wa kuwepo kwa mivutano ya madaraka ndani ya safu za uongozi wake, akisisitiza dhamira yake ya kusalia kama kiongozi mkuu pekee wa taifa hilo. Traore aliwaambia viongozi wa jamii hivi karibuni mjini Ouahigouya, kaskazini mwa nchi hiyo kwamba: “Meli haiwezi kuwa na manahodha wawili,”

Kutokuwepo kwa muda mrefu kwa viongozi wawili wa ngazi za juu kumechochea minong’ono ya kuwepo kwa msuguano ndani ya serikali hiyo, ambayo iliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mnamo Septemba 2022.

Naibu wake, Oumarou Yabre, ni mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika mfumo wa usalama wa Burkina Faso. Ofisa mmoja wa usalama amebainisha kuwa Yabre ameacha kuonekana katika ofisi yake katika Shirika la Kitaifa la Ujasusi, na ulinzi uliokuwa umepewa makazi yake umepunguzwa kwa kiasi kikubwa. Farouk Azaria Sorgho, msemaji wa jeshi na kamanda wa Kikosi cha Uingiliaji Kati cha Haraka (Rapid Intervention Battalion), ndiye kiongozi wa tatu kwa cheo. Amekuwa na jukumu kuu katika kusafisha utawala wa umma, akikemea vitendo vya utovu wa nidhamu wa kifedha na kutekeleza adhabu kali. Hata hivyo, tangu katikati ya mwezi Mei, Kikosi Namba 4 kimekuwa kikiendeshwa na naibu wa Sorgho, huku maafisa wa usalama wakidai kuwa kamanda huyo amewekwa kizuizini na washirika wa Traore. Watu wote wawili hawajaonekana hadharani tangu mwezi Mei.

Kapteni huyo mwenye umri wa miaka 38 amesisitiza: “Kila anayefanya kazi nami anajua jinsi ninavyoendesha mambo.”

Akaonya: “Yeyote atakayeenda kinyume na misingi, nitamwajibisha bila kusita. Hakuna mababe wanaonizunguka.”

Wakati huo huo, operesheni za kiusalama zimeimarishwa zaidi katika mji mkuu, Ouagadougou, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Wakazi wa eneo hilo wanasema kuwa barabara zilizokuwa zimefungwa kwa miaka mingi zimefunguliwa upya ili kuelekeza trafiki mbali na ikulu ya rais, ambapo vizuizi vya ukaguzi wa kiusalama vimewekwa. Serikali ya Burkina Faso imeituhumu Ufaransa mara kadhaa kwamba inapanga njama ya kumpindua Kapteni Traore ambaye amechukua misimamo imara ya kupinga  ukoloni mambo-leo wa Paris.