Ripoti: Tathmini ya CIA yakiri hujuma za Marekani dhidi ya Iran zimeshindwa
-
Ripoti: Tathmini ya CIA yakiri hujuma za Marekani dhidi ya Iran zimeshindwa
Tathmini mpya ya kiintelijensia ya Marekani imetoa pigo kubwa kwa propaganda za kivita za utawala wa Donald Trump, kwa kuhitimisha kwamba kuendelezwa kwa uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hakutaweza kufanikisha malengo yoyote yaliyotangazwa na Ikulu ya White House.
Kwa mujibu wa ripoti ya The Washington Post, tathmini hiyo, iliyoandaliwa kwa kiasi kikubwa na CIA, inakiri kwamba licha ya siku kadhaa za mashambulizi ya anga yasiyokoma, Iran imesalia imara katika misimamo yake kuhusu vikwazo, haki zake za kisheria na za kujitawala, pamoja na usalama katika lango la kimkakati la Hormuz.
Matokeo hayo yamekuja wakati Marekani ikiendeleza mashambulizi ya karibu wiki mbili dhidi ya Iran, kufuatia tangazo la upande mmoja la Rais Donald Trump la kumalizika kwa mapatano ya usitishaji vita.
Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya Wairan kadhaa, wakiwemo watoto, huku wanajeshi watatu wa Marekani wakiuawa katika operesheni za kulipiza kisasi za Iran. Vikosi vya Marekani vimeshambulia maeneo mengi ya Iran katika kipindi cha wiki mbili ikiwemo miundombinu ya kiraia kama madaraja, reli, hospitali, mabomba ya maji safi na vituo vya umeme.
Vita hivyo tayari vimeanza kupanuka na kuwa mzozo mpana wa kikanda, huku Yemen ikitangaza kuzia baadhi ya meli za mafuta katika Lango Bahari la Bab al-Mandab katika Bahari ya Sham.
Kufungwa kwa Lango la kimkakati la Hormuz kumesukuma akiba ya kimkakati ya mafuta ghafi ya Marekani kushuka hadi kiwango chake cha chini zaidi tangu mwaka 1983, wakati wastani wa bei ya petroli kote nchini humo umevuka dola 4 kwa galoni.
Tathmini ya CIA imefichua “kinamasi” alichotumbukia Rais Trump kutokana na vita vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran vilivyoanzishwa mwezi Februari.
Naibu wa zamani wa afisa wa ujasusi wa kitaifa, Jonathan Panikoff, alihoji mkakati wa utawala huo akiliambia gazeti la Washington Post: “Utawala wa Trump unaonekana kuamini kwamba ukiendelea kuishambulia Iran kwa nguvu zaidi kijeshi, Tehran hatimaye itakuwa tayari kulegeza msimamo. Tathmini hiyo bila shaka si sahihi.”
Ripoti hiyo imesisitiza kuwa Iran “haitahisi athari kubwa” licha ya mashambulizi mazito ya anga ya Marekani.
Tathmini za awali za kiintelijensia za mwezi Aprili zilizonukuliwa na CNN zilionyesha kuwa Tehran “bado inadumisha uwezo mkubwa wa kurusha makombora” licha ya mashambulizi ya Marekani na Israel, huku chanzo kimoja kikisema vikosi vya Iran “bado viko katika hali ya utayari mkubwa wa kusababisha msukosuko mkubwa kabisa katika eneo zima.”