Dkt. Mwigulu Nchemba ateuliwa Waziri Mkuu mpya wa Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133114-dkt._mwigulu_nchemba_ateuliwa_waziri_mkuu_mpya_wa_tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan leo amewasilisha bungeni jina la Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya wa serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(last modified 2025-11-13T12:37:37+00:00 )
Nov 13, 2025 06:22 UTC
  • Dkt. Mwigulu Nchemba ateuliwa Waziri Mkuu mpya wa Tanzania
    Dkt. Mwigulu Nchemba ateuliwa Waziri Mkuu mpya wa Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan leo amewasilisha bungeni jina la Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya wa serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Spika Mussa Zungu alipokea hati ya uteuzi huo kutoka kwa Rais Samia na kulijulisha kwa wabunge kwa ajili ya kumthibitisha kwa kura kwa mujibu wa ibara ya 51 kifungu kidogo cha pili.

Rais Samia, amelipendekeza jina la Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uteuzi huo unafanyika kufuatia taratibu za kikatiba ambapo jina la mgombea huwasilishwa kwa Bunge la Tanzania ili kupigiwa kura na wabunge.

Baada ya pendekezo hilo, wabunge watapiga kura ili kuthibitisha au kukataa uteuzi wa Mwigulu Nchemba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwigulu anakuwa Waziri wa 12 tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania.

Mwigulu ni mchumi, kada wa muda mrefu wa chama cha mapinduzi, (CCM) akimrithi Kassim majaliwa anayemaliza muda wake. Mwanasiasa huyo wa muda mrefu, alikuwa Waziri wa Fedha katika serikali ya Samia.

Mwigulu Lameck Nchemba Madelu ni mwanasiasa Mtanzania na mwanachama wa chama cha kisiasa cha CCM ambaye amekuwa waziri wa fedha na mipango tangu 31 Machi 2021.

Alisoma uchumi kwenye Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam alipohitimu shahada ya uzamili mwaka 2006.