Larijani: Hakuna ujumbe mpya uliotumwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133082-larijani_hakuna_ujumbe_mpya_uliotumwa_marekani
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amepuuzilia mbali ripoti kwamba kumekuwepo mawasiliano mapya kati ya Tehran na Washington na kusisitiza kuwa hakuna ujumbe mpya uliowasilishwa kwa Marekani.
(last modified 2025-11-12T07:38:23+00:00 )
Nov 12, 2025 07:38 UTC
  • Ali Larijani
    Ali Larijani

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amepuuzilia mbali ripoti kwamba kumekuwepo mawasiliano mapya kati ya Tehran na Washington na kusisitiza kuwa hakuna ujumbe mpya uliowasilishwa kwa Marekani.

Ali Larijani amesisitiza kuwa kipaumbele cha Iran ni kuondolewa vikwazo dhidi yake, ambako amekutaja kuwa ndilo lengo kuu la juhudi za kidiplomasia za serikali.

Larijani amesema hakuna jumbe zozote mpya zilizotumwa kwa Washington kwa kuzingatia kuwa mazungumzo ya awali yalikuwa yamefanyika, lakini Marekani haikuonyesha nia ya kufikia makubaliano.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amebainisha haya baada ya kuenea tetesi kuhusu mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington kuhusu kadhia ya nyuklia na masuala ya kikanda. 

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa kuondolewa vikwazo ni msingi wa hatua yoyote ya kidiplomasia, hata hivyo Marekani imeshindwa kuonyesha nia ya kweli ya kufikia makubaliano. 

Iran na Marekani zilikuwa zimefanya duru tano za mazungumzo hadi mwanzoni mwa mwaka huu ili kupata mbadala wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015. Hata hivyo Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi ya siku 12 dhidi ya ardhi ya Iran kabla kidogo ya kufanyika duru ya sita ya mazungumzo na kuuwa mamia ya watu na kuharibu miundo mbinu ya kijeshi na taasisi za kuzlisha nishati ya nyuklia.