Mazungumzo ya simu kati ya Vladimir Putin na Masoud Pezeshkian
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137210-mazungumzo_ya_simu_kati_ya_vladimir_putin_na_masoud_pezeshkian
Rais wa Russia, Vladimir Putin, amefanya mazungumzo ya simu na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo, ambapo Rais wa Iran amesisitiza kuwa: “ Njia yetu ni kujihami kwa nguvu ili kulinda mipaka yetu na kuleta amani endelevu.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Mar 07, 2026 04:07 UTC
  • Mazungumzo ya simu kati ya Vladimir Putin na Masoud Pezeshkian

Rais wa Russia, Vladimir Putin, amefanya mazungumzo ya simu na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo, ambapo Rais wa Iran amesisitiza kuwa: “ Njia yetu ni kujihami kwa nguvu ili kulinda mipaka yetu na kuleta amani endelevu.

Kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya Rais wa Iran, Pezeshkian katika mazungumzo hayo ya simu ameashiria mashauriano ya kidiplomasia na nchi za kanda, na kusema: “Tumewafafanulia majirani zetu kwamba kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani ni hatua ya kujilinda tu na inafanywa kwa ajili ya kulinda nchi na watu wetu.”

Katika mazungumzo hayo, Rais amesema mauaji ya kinyama ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kitendo kinachokiuka sheria zote na kanuni za kimataifa. Ameongeza kuwa: “Madola ya kibeberu yanajaribu kullazimisha matakwa yao kwa mataifa kwa kutumia mabavu, lakini mahudhurio ya mamilioni na ya kishujaa ya taifa la Iran katika kuunga mkono mfumo na nchi yao yamethibitisha kuwa mashambulizi haya yanazidi tu kuimarisha azma ya taifa letu katika kulinda uhuru wa nchi.”

Rais Pezeshkian, amekumbusha tena  maonyo yake ya awali kuhusu kutouamini upande wa pili na kuongeza kuwa:  “Katika mawasiliano yetu ya mwisho, ulieleza kwamba kulingana na madai ya Netanyahu, hawana nia ya kuishambulia Iran. Hata hivyo, leo imedhihirika kwa wote kwamba uongo na nia mbaya ni sehemu ya asili yao, na katikati ya ahadi za mazungumzo, wamevamiwa tena.”

Rais wa Iran amesisitiza kuwa kuna matarajio makubwa kuwa Russia itatumia uwezo wake wote wa kimataifa kusaidia na kutetea haki za kisheria za taifa la Iran dhidi ya vitendo hivi vya uvamizi.

Dkt. Pezeshkian, akirejelea mazungumzo yake ya kidiplomasia na nchi za kanda, amesema: “Tuliwaelezea majirani zetu katika mawasiliano yetu kuwa kulenga kambi za kijeshi za Marekani kulikuwa ni hatua ya kulinda taifa na wananchi. Mashambulizi ya hivi karibuni kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni yamethibitisha tena ukweli wa msimamo wa Tehran: kwamba usalama wa kanda unaweza kuhakikishwa tu na nchi za ukanda wenyewe, na kwamba uwepo wa vikosi vya kigeni ndio kiini na chanzo kikuu cha ukosefu wa amani.”

Rais Pezeshkian amepinga kwa nguvu madai yaliyotolewa kuhusu shambulio dhidi ya Jamhuri ya Azerbaijan, na kusema kuwa uvumi huo umeenezwa na maadui kwa lengo la kuvunja uhusiano wa na majirani wetu.

Amesisitiza kwamba: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuwa na nia ya kuvamia nchi jirani." 

Rais Pezeshkian ametoa shukrani zake kwa serikali na taifa la Russia kwa kujali hali ya Iran hivi sasa na ameonyesha matumaini yake kwamba nchi huru na mashirika ya kimataifa, kwa kuunganisha nguvu, watalazimisha nchi za kibeberu  kutii sheria na kuheshimu haki za binadamu na za mataifa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Vladimir Putin ametoa tazia zake za dhati kutokana na kuuawa shahidi Kiongozi Muadhamu  wa Mapinduzi ya Kiislamu na akaelezea huruma yake kuu kwa serikali na watu wa Iran. Akirejelea mawasiliano yake ya mara kwa mara na viongozi wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi, Rais Putin alisisitiza umuhimu wa amani uthabiti katika ukanda huu.

Hatimaye, marais wa nchi hizi mbili wamekubaliana kuwa uratibu baina ya Tehran na Moscow utaendelea kwa kasi na uthabiti kupitia njia mbalimbali za kidiplomasia na kiusalama.