Pezeshkian: Iran imesimama kidete katika kujihami, kulinda heshima ya taifa
Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haitasita kuendelea kujihami na kujilinda mkabala wa mashambulizi ya kichokozi ya maadui wa taifa hili.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran la Mehr, Masoud Pezeshkian, Rais wa Iran, amesema hayo kwenye ujumbe alioutuma leo kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X na kubainisha kuwa, "Tumejitolea kwa ajili ya amani ya kudumu katika eneo (la Asia Magharibi), lakini tumesimama kidete kulinda heshima ya taifa hili."
Rais wa Iran ameeleza kuwa, baadhi ya nchi zimeanzisha juhudi za upatanishi, ili kupunguza taharuki iliyopo na kueleza bayana kuwa, jibu la Iran kwa jitihada hizo liko wazi.
Dakta Pezeshkian amebainisha kuwa, "Wanaotaka kuwa wapatanishi wanapasa kwenda kwa wale waliotweza na kudunisha uwezo na nguvu za taifa la Iran." Rais wa Iran amezihutubu tawala za Marekani na Israel kwa kuwasha moto ambao haziwezi kuuzima na kuziambia kwamba: Kwa kudunisha uwezo wa taifa hili, mumewasha moto wa mzozo uliopo.
Kabla ya hapo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema katika ujumbe wake kwa viongozi wa nchi rafiki na majirani kwamba, mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel yameiacha Iran bila chaguo lolote isipokuwa kujilinda.
Vikosi vya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinaendeleza operesheni za ‘Ahadi ya Kweli 4’ ikiwa ni katika kujibu uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ulioanzishwa Jumamosi iliyopita ya Februari 28.
Operesheni hizo za kijeshi za Iran zimeendelea kulenga ngome za kijeshi, kiuchumi na kisiasa za utawala wa Kizayuni wa Israel na vituo vya kijeshi na kijasusi vya Marekani katika ardhi za nchi za eneo hili.