Mohsen Rezaei: Tutaifukuza Marekani kutoka Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137188-mohsen_rezaei_tutaifukuza_marekani_kutoka_ghuba_ya_uajemi
Kamanda wa zamani wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amezungumzia matukio ya hivi karibuni ya vita na kusema: “Wananchi wa Iran wanapaswa kufahamu kwamba wana wao walioko katika vikosi vya ulinzi wako tayari kuwafundisha wahalifu Donald Trump na Benjamin Netanyahu funzo kali kiasi kwamba hawatathubutu tena kufanya jeuri ya aina hii.”
(last modified 2026-03-06T03:50:34+00:00 )
Mar 06, 2026 03:50 UTC
  • Meja Jenerali Mohsen Rezaei
    Meja Jenerali Mohsen Rezaei

Kamanda wa zamani wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amezungumzia matukio ya hivi karibuni ya vita na kusema: “Wananchi wa Iran wanapaswa kufahamu kwamba wana wao walioko katika vikosi vya ulinzi wako tayari kuwafundisha wahalifu Donald Trump na Benjamin Netanyahu funzo kali kiasi kwamba hawatathubutu tena kufanya jeuri ya aina hii.”

Meja Jenerali Mohsen Rezaei ameyasema hayo katika mahojiano ya Chaneli ya Habari ya IRIB ambapo kwanza ametoa salamu za rambirambi kwa kufa shahidi na kishujaa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khamenei, kwa umma unaothamini mashahidi na kwa Waislamu wote duniani. Akiwahutubia wananchi wa Iran amesema: “Kisasi kikali ambacho tumekianza dhidi ya Marekani na Israel kitaendelea. Kama alivyosisitiza Kiongozi Muadhamu, tutawaweka katika hali ya kukata tamaa na kuwapa funzo ambalo hawatalisahau kamwe.”

Ameongeza kuwa: “Kuuawa shahidi Imam Khamenei kutafungua ukurasa mpya katika historia ya nchi, ukurasa ambao ndani yake mamlaka na usalama wa Iran vitaimarishwa na matatizo yetu yataondoka. Wakati huohuo, tukio hili limeonesha kwa uwazi kilele cha uovu wa Marekani na utawala wa Kizayuni.”

Ameongeza kuwa ni vigumu kuamini kwamba kuanzia sasa baadhi ya nchi zitaweza tena kufikiria kuwa na uhusiano na Marekani kwa heshima na hadhi.

Jenerali Rezai ambaye alikuwa Kamanda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi cha Vita vya Kujihami Kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran kuanzia 1980-88)  pia ameashiria kauli za baadhi ya viongozi wa Ulaya wanaodai kutounga mkono shambulio dhidi ya Iran, akisema: “Kuanzia leo hali ya mambo inaanza kubadilika. Mataifa ya dunia yanafurahia kuona kwamba kuna nchi iliyojitokeza kuikabili Marekani waziwazi.” Ameongeza kuwa, kuanzia sasa Iran itakuwa kimbilio la mataifa mengi na itapata nafasi kubwa zaidi katika ulingo wa kimataifa.

Kamanda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amefafanua kuhusu hali ya uwanja wa vita akisema: Katika vita vya sasa tumepata mafanikio mazuri katika nyanja za kijeshi, ambapo kwa mfano tumetungua makumi ya ndege zisizo na rubani za kisasa za Marekani na Israel. Aidha amesema: “Takribani wanajeshi 700 wa Marekani wameuawa au kujeruhiwa; vituo kadhaa vya kijeshi, kwa mujibu wa kauli zao wenyewe, vimeharibiwa.”

Ameongeza kuwa kwa sasa upungufu wa mifumo ya ulinzi wa anga ya Marekani umefikia kiwango cha kulazimika kufikiria kuhamisha mifumo hiyo kutoka Asia ya Mashariki.

Jenerali Rezaei pia ameashiria kauli za Trump kwamba wanaweza kuendelea na vita kwa wiki kadhaa, akisema: “Kauli hiyo ni uongo mkubwa. Kwa upande mwingine, amesema Benjamin Netanyahu alimshawishi vibaya Trump kwa kumwambia kuwa operesheni ingeweza kumalizika ndani ya saa 48.”

Amesema Marekani na Israel hazina uwezo wa kuendesha vita vya muda mrefu, ilhali Iran ina uwezo huo. Amesema kuwa uzoefu wa vita vya miaka minane ulionyesha kwamba pale heshima ya kisiasa ya Iran inapokuwa hatarini, nchi hii huchukua hatua kali. Amesema, vita hivyo vilileta karibu miongo minne ya usalama kwa Iran; na safari hii, amesisitiza kuwa mchakato wa kujihami hautasitishwa isipokuwa “kuikomboa Ghuba ya Uajemi” na kuondoa uwepo wa Marekani katika eneo hilo.