Binti wa Zuma akana mashtaka ya uchochezi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133028-binti_wa_zuma_akana_mashtaka_ya_uchochezi
Duduzile Zuma-Sambudla, bintiye rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amekana mashtaka ya kuchochea ghasia wakati wa machafuko makubwa yaliyotokea nchini humo mwezi Julai 2021.
(last modified 2025-11-11T02:52:07+00:00 )
Nov 11, 2025 02:52 UTC
  • Duduzile Zuma-Sambudla
    Duduzile Zuma-Sambudla

Duduzile Zuma-Sambudla, bintiye rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amekana mashtaka ya kuchochea ghasia wakati wa machafuko makubwa yaliyotokea nchini humo mwezi Julai 2021.

Duduzile Zuma Sambludla jana Jumatatu alifikishwa Mahakama Kuu katika kikao cha kwanza cha kusikiliza kesi inayomkabili katika mji wa Durban ambapo waendesha mashtaka walidai kuwa machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii yalichochea watu wengine kujihusisha na vitendo vya ukatili na hivyo kuzidisha machafuko ambayo yaliikumba nchi hiyo katika kipindi hicho cha msukosuko. 

Duduzile amekanusha tuhuma dhidi yake katika Mahakama Kuu ya Durban huku akiwa amevalia fulana yenye maneno: "Modern Day Terrorist" -ambayo yametajwa kuwa ni ukosoaji kwa tuhuma zilizowasilishwa dhidi yake. 

Ghasia hizo zilichochewa na kufungwa jela Jacob Zuma kufuatia kesi ya ufisadi iliyokuwa ikimkabili. Ghasia zilizoanza katika eneo la KwaZulu-Natal zilienea kwa kasi hadi Gauteng na kusababisha uporaji mkubwa, kuchomwa moto milki za umma na vifo vya zaidi ya watu 300 na kuharibiwa pakubwa biashara.

Zuma-Sambudla alimfuata babake alipohama chama tawala cha African National Congress mwaka 2023 na kujiunga na uMkhonto weSizwe (MK); chama cha kizalendo kilichopewa jina la mrengo wa zamani wa tawi la kijeshi la ANC.