Iran yaadhimisha Siku ya Arobaini ya Mashahidi wa ghasia za kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136734-iran_yaadhimisha_siku_ya_arobaini_ya_mashahidi_wa_ghasia_za_kigaidi
Wairani leo wanashiriki katika hafla kubwa ya kitaifa mjini Tehran kuadhimisha siku ya arobaini tangu kuuawa kishahidi kwa watu waliopoteza maisha yao katika mashambulizi ya kigaidi ya Januari 8 na 9.
(last modified 2026-02-17T10:42:53+00:00 )
Feb 17, 2026 10:42 UTC
  • Iran yaadhimisha Siku ya Arobaini ya Mashahidi wa ghasia za kigaidi

Wairani leo wanashiriki katika hafla kubwa ya kitaifa mjini Tehran kuadhimisha siku ya arobaini tangu kuuawa kishahidi kwa watu waliopoteza maisha yao katika mashambulizi ya kigaidi ya Januari 8 na 9.

Kwa mujibu wa Baraza la Uratibu wa Uenezaji wa Uislamu, hafla hiyo imelenga kuheshimu damu safi ya mashahidi na subira ya familia zao, waliotoa mchango mkubwa katika kulinda usalama wa nchi.

Baraza hilo lilielezea matukio ya mapema Januari kuwa ni operesheni ya mseto na ya kifikra (hybrid and cognitive operation) iliyopangwa na maadui wa taifa kwa lengo la kudhoofisha usalama wa kisaikolojia wa jamii ya Iran.

Katika taarifa yake, baraza hilo lilisema kuwa ingawa baadhi ya makundi yalijaribu kuyatumia malalamiko halali ya wananchi kwa kuwatumia mawakala wa takfiri na kigaidi, maandamano ya kimapinduzi ya wananchi wa Iran tarehe 11 Januari yalifanikiwa kubatilisha njama hizo za maadui.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa ushiriki wa makundi mbalimbali ya kijamii katika hafla hiyo utaleta faraja kwa familia za mashahidi na wakati huohuo kuimarisha kinga ya kitaifa dhidi ya njama za baadaye.

Katika taarifa tofauti, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesisitiza kuwa maadhimisho ya siku ya arobaini ni hatua ya kimkakati ya kutathmini mapambano makubwa katika “vita vya irada”.

IRGC imeyataja matukio ya Januari 8 na 9, 2026, kuwa ni njama ya hali ya juu iliyolenga kuunda machafuko yaliyoratibiwa na kuyumbisha uthabiti wa nchi, ili kuandaa mazingira ya hujuma ya kigeni na hatimaye kusambaratisha nchi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, operesheni hizo zilizofanywa na magaidi wenye silaha ziliongozwa na Mossad na CIA, zikichanganywa na vita vya kisaikolojia, udhibiti wa vyombo vya habari, na juhudi za kuvuruga mzunguko wa utawala wa nchi.

IRGC iliongeza kuwa mkakati huo ulihusisha kueneza hofu, kuharibu miundombinu, na kutekeleza kile ilichokiita “miradi ya mauaji” kwa lengo la kuchochea hisia za umma, hususan miongoni mwa vijana.

Mapema Januari, rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ametishia Iran kwa mashambulizi iwapo serikali  ingewadhuru magaidi ambao aliwaita “waandamanaji wa amani.”

Siku chache baadaye, tarehe 8 na 9 Januari, makundi yenye silaha yalianzisha mashambulizi ya pamoja dhidi ya vituo vya polisi, kambi za kijeshi, maeneo nyeti ya serikali, pamoja na miundombinu ya kiraia katika miji kadhaa.

Maafisa wa Iran wamesema mashambulizi hayo yalilenga kusababisha vifo vya watu wengi na kuyumbisha vituo vya mijini kote nchini.

Maafisa hao pia wamekosoa mara kwa mara vyombo vya habari vya Magharibi kwa kusambaza takwimu zisizo sahihi za vifo na kuilaumu serikali ya Iran.

Baadhi ya ripoti za Kimagharibi zimedai kuwa hadi watu 30,000 waliuawa kufuatia kile walichokiita “maandamano ya amani.”

Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu rasmi za Iran, jumla ya watu 3,117 walipoteza maisha katika ghasia hizo, wakiwemo raia 2,427 pamoja na wanajeshi na maafisa wa usalama, waliouawa na makundi ya kigaidi.