Idadi ya vifo vya Kimbunga Gezani yapanda hadi 59 nchini Madagascar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136732-idadi_ya_vifo_vya_kimbunga_gezani_yapanda_hadi_59_nchini_madagascar
Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia Kimbunga Gezani nchini Madagascar imeongezeka hadi 59, huku watu 804 wakijeruhiwa. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Ofisi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Hatari na Maafa (BNGRC).
(last modified 2026-02-17T10:41:28+00:00 )
Feb 17, 2026 10:41 UTC
  • Idadi ya vifo vya Kimbunga Gezani yapanda hadi 59 nchini Madagascar

Idadi ya watu waliopoteza maisha kufuatia Kimbunga Gezani nchini Madagascar imeongezeka hadi 59, huku watu 804 wakijeruhiwa. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Ofisi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Hatari na Maafa (BNGRC).

BNGRC imetangaza kuwa zaidi ya watu 420,000 wameathiriwa katika wilaya 25 ndani ya mikoa mitano ya mashariki na kati mwa nchi hiyo.

Kimbunga hicho pia kimeharibu zaidi ya nyumba 49,000 na kuangamiza kabisa zaidi ya nyumba 25,000, na kuwaacha maelfu ya familia bila makazi.

Kwa mujibu wa mamlaka husika, tathmini ya uharibifu bado inaendelea, sambamba na operesheni za uokoaji na misaada ya dharura katika maeneo yaliyoathiriwa, huku msaada wa kibinadamu ukiendelea kuwafikia wananchi waliopatwa na janga hilo.

Serikali ya Madagascar imetangaza hali ya janga la kitaifa (state of national disaster) kuanzia Februari 11, kufuatia uharibifu mkubwa uliosababishwa na Kimbunga Gezani.

Maafisa wamesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa na wa kimataifa katika kusaidia waathirika, wakieleza kuwa juhudi za pamoja zinahitajika ili kupunguza madhara ya kibinadamu na kurejesha maisha ya kawaida katika maeneo yaliyoathiriwa.

Kwa mujibu wa taarifa za hali ya hewa, kimbunga hicho kiliundwa katika Bahari ya Hindi wiki iliyopita na kuvuka Madagascar, kikisababisha vifo vya zaidi ya watu 59 katika awamu za awali. Kulikuwepo na hofu kwamba Gezani ingeikumba pia Msumbiji, lakini hakikutua katika pwani ya nchi hiyo.

Hata hivyo, kimbunga hicho kilisababisha upepo mkali na mvua kubwa katika maeneo ya Inhambane na mkoa wa Sofala nchini Msumbiji. Kwa mujibu wa Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, watu wanne walipoteza maisha wakati wa kupita kwa Kimbunga Gezani katika maeneo hayo.

Maafisa wa kikanda wamehimiza ushirikiano wa kibinadamu na maandalizi ya pamoja katika ukanda wa Bahari ya Hindi, wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya tahadhari mapema ili kupunguza madhara ya majanga ya asili yanayozidi kuongezeka.