Kikosi cha Majini cha IRGC chafanya luteka Ghuba ya Uajemi, Hormuz
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136714-kikosi_cha_majini_cha_irgc_chafanya_luteka_ghuba_ya_uajemi_hormuz
Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, Iran inadumisha ufuatiliaji kamili wa kijasusi wa saa 24 katika Lango-Bahari la Hormuz.
(last modified 2026-02-17T02:58:31+00:00 )
Feb 17, 2026 02:58 UTC
  • Kikosi cha Majini cha IRGC chafanya luteka Ghuba ya Uajemi, Hormuz

Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba, Iran inadumisha ufuatiliaji kamili wa kijasusi wa saa 24 katika Lango-Bahari la Hormuz.

Akizungumza wakati wa mazoezi ya jeshi la majini la IRGC katika Ghuba ya Uajemi, Admeli Alireza Tangsiri amesisitiza kwamba, "usimamizi huu kamili" unalenga kuhakikisha usalama wa usafiri kupitia njia ya kimkakati ya majini.

Amebainisha kuwa, uchumi wa mataifa ya Asia Magharibi na mataifa mengi yana mafungamano na usalama wa mshipa huu muhimu wa baharini. Kamanda huyo ameelezea visiwa vya Iran katika Ghuba ya Uajemi na Mlango-Bahari wa Hormuz kama "heshima ya kitaifa" na akavitaja kama "ngome na meli za kivita zisizoweza kupenyeka."

Admeli Tangsiri ameongeza kuwa, ingawaje maneva haya ni matukio ya kawaida ya kila mwaka, lakini ya mara hii ni maalum kwa ajili ya kuzinduliwa mbinu mpya na suhula maalum. Amesema, "Tunaonyesha baadhi ya maendeleo haya kupitia vyombo vya habari, huku sehemu kubwa ikibaki kuainishwa kwa ajili ya kufichuliwa baadaye."

Awamu ya kwanza ya luteka hii imefanywa kwa mafanikio katika visiwa vya Iran katika Ghuba ya Uajemi siku ya Jumatatu. Mazoezi hayo yalihusisha vipengele kadhaa muhimu.

Droni za Iran katika luteka Ghuba ya Uajemi

Vikosi maalum vya kukabiliana haraka na maadui vilifanya mazoezi ya kwa kutumia mbinu za kisasa za kushambulia na kujilinda. Operesheni za makombora pia zilifanywa kwa kutumia aina mpya zaidi za makombora, zikizingatia mbinu za mapigano ndani ya mazingira ya vita vya kielektroniki (EW).

Droni na silaha za chini ya ardhi pia zilizinduliwa katika visiwa vitatu vya Iran vya Tunb Kubwa, Tunb Ndogo na Abu Mosa ili kushambulia shabaha dhahania zilizoanishwa.

Awamu kuu ya mazoezi hayo ya kijeshi imepangwa kufanyika leo Jumanne katika Lango-Bahari la Hormuz, ikizingatia udhibiti mzuri wa njia hiyo ya kimkakati ya majini.